Kilichomtokea Dk. Shein mjini Moroni na fasili ya kisheria
Kessy, ni wabunge wa Tanganyika wapaswao kutoka kuunda bunge lao
KMKM Pemba, hamuviwezi vita dhidi ya mwanamke mwenye haki
U.S. Democracy Promotion in Africa: Why Zanzibar Matters
Mwenye mizinga na mwenye umma, nani hasa mwenye nguvu?
“Tanganyika inaidhibiti Zanzibar kijeshi na kisiasa”
“Kilele cha matumizi haya ya mabavu ya kijeshi ni Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, ambako vibaraka wa Tanganyika katika Zanzibar walikataliwa kabisa na wananchi wa Zanzibar katika Uchaguzi wa Rais, Wawakilishi na Madiwani. Ni Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) tu ndilo ambalo limehakikisha kwamba vibaraka hawa waliokataliwa na wananchi wao, wanaendelea kubakia madarakani.”
MAONI YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI, WIZARA YA KATIBA NA SHERIA, MHESHIMIWA TUNDU A.M. LISSU (MB.) KUHUSU MPANGO NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA YA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA KWA MWAKA 2016/2017
(Kanuni ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, 2016)
UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,
Kabla ya kufanya kazi ambayo ninatakiwa kuifanya kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge lako tukufu na ambayo umeniitia, naomba – kwa ridhaa yako – niseme maneno machache juu ya jambo binafsi linalonihusu mimi na familia yangu. Tarehe 7 Aprili, 2016, aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Singida katika Bunge la Kumi, Mheshimiwa Christina Lissu Mughwai, alifariki dunia katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam. Marehemu alikuwa dada yangu na mdogo wangu wa kuzaliwa.
Kufuatia kifo chake, na licha ya kuwa hakuwa Mbunge tena, uongozi wa Bunge lako tukufu ulichukua jukumu la kuhakikisha Marehemu Christina Mughwai anazikwa kwa heshima zote zinazostahili Mbunge. Waheshimiwa Wabunge – kwa namna mbali mbali – walishiriki katika kuhakikisha mpendwa wetu anapata mazishi ya heshima kubwa. Baadhi yenu hata mlifunga safari ya kumsindikiza Marehemu hadi nyumbani kwetu Kijiji cha Mahambe, Wilaya ya Ikungi ambapo mazishi yalifanyika tarehe 13 Aprili, 2016.
Na sio Bunge na Waheshimiwa Wabunge tu. Serikali ya Jamhuri ya Muungano, ikiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano mwenyewe, Dkt. John Pombe Magufuli, ilishiriki moja kwa moja katika mazishi hayo. Licha ya shughuli zake nyingi, Rais mwenyewe alikuja kuupokea mwili wa Marehemu na kutoa heshima zake katika Ukumbi wa kihistoria wa Karimjee. Na baadae kwenye mazishi nyumbani kwetu Mahambe, Rais alimtuma Waziri wake, Mheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba, kuja kuiwakilisha Serikali katika mazishi hayo. Tulipata kila aina ya msaada tuliohitaji kutoka kwa Bunge, Serikali na Waheshimiwa Wabunge. Hatukuwa wapweke. Hamkutuacha peke yetu katika majonzi yetu. Mlilia na sisi, na mlitufuta machozi. Mlitufariji sana katika kipindi chote cha kilio chetu. Mliufanya msiba wetu kuwa msiba wenu.
Kwa sababu zote hizi, Mheshimiwa Spika, nimetumwa na waliomzaa na kumlea Marehemu Christina Mughwai; nimeagizwa na ndugu zake na marafiki zake na jirani zake, kutoa shukrani zao za dhati kabisa kwa uongozi wa Bunge lako tukufu, kwa Waheshimiwa Wabunge wote na kwa Rais na Mama John Pombe Magufuli na Serikali yake yote, kwa ajili ya wema na upendo na heshima mliyotupatia wakati wa mazishi ya mpendwa wetu Christina Lissu Mughwai. Mwenyezi Mungu awazidishie pale mlikopungukiwa na awabariki sana.
Baada ya kusema haya, Mheshimiwa Spika, sasa naomba nitimize wajibu wangu wa kibunge kama Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu kuhusu hoja iliyoko mezani. Na naomba niweke wazi mapema kwamba nitakayoyasema hapa hayatawafurahisha wengi, ndani na nje ya Ukumbi huu wa Bunge lako tukufu. Hata hivyo, kama alivyosema Frederick Douglass, babu wa harakati za kudai haki za watu weusi wa Marekani ya wakati wa utumwa wa Waafrika zaidi ya miaka mia moja na hamsini iliyopita, “he is a lover of his country who rebukes its sins rather than justify them”, yaani, “ni mpenzi wa nchi yake yule anayekemea madhambi yake badala ya kuyahalalisha.”
UTAWALA BILA SHERIA!
Mheshimiwa Spika,
Tarehe 15 Aprili, 1980, Bunge hili lilitunga Sheria ya Utekelezaji wa Majukumu ya Kiuwaziri, Sheria Na. 10 ya 1980. Sheria hiyo ilipata ridhaa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na kuanza kutumika Mei Mosi ya 1980. Pamoja na mambo mengine, Sheria hiyo ilimpatia mamlaka ya kuainisha idara, shughuli na mambo mengine ambayo kwayo kazi na majukumu yake amebaki nayo yeye mwenyewe au ameyakasimu kwa Mawaziri na tarehe ya kuanza kutekeleza majukumu hayo.
Tangu wakati huo, imekuwa ni sheria, na sehemu ya mila na desturi ya kikatiba ya nchi yetu, kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano kuainisha – kwa kupitia Tangazo lililochapishwa katika Gazeti la Serikali – Wizara, idara, shughuli na mambo mengine ambayo Rais amejibakizia mwenyewe, na yale ambayo amekasimu majukumu yake kwa Mawaziri. Utafiti wetu unaonyesha mambo yafuatayo katika miaka 36 na ya utekelezaji wa Sheria hii:
- Mwaka 1981, Rais Nyerere alitoa Tangazo la Ukasimishaji wa Majukumu ya Kiuwaziri la mwaka 1981 (The Ministers [Assignment of Ministerial Functions] Notice, 1981, ambalo lilichapishwa katika Gazeti la Serikali kama Tangazo la Serikali Na. 16 la tarehe 6 Februari, 1981;
-
Mwaka 1986, Rais Ali Hassan Mwinyi alitoa Tangazo la Ukasimishaji wa Majukumu ya Kiuwaziri la mwaka 1986 (The Ministers [Assignment of Ministerial Functions] Notice, 1986), ambalo lilichapishwa katika Gazeti la Serikali kama Tangazo la Serikali Na. 29 la 1986;
-
Mwaka 2000, Rais Benjamin William Mkapa alitoa Tangazo la Ukasimishaji wa Majukumu ya Kiuwaziri la mwaka 2000 (The Ministers [Assignment of Ministerial Functions] Notice, 2000), ambalo lilichapishwa katika Gazeti la Serikali kama Tangazo la Serikali Na. 468 la 2000;
-
Mwaka 2006 Rais Jakaya Mrisho Kikwete alitoa Tangazo la Ukasimishaji wa Majukumu ya Kiuwaziri la mwaka 2006 (The Ministers [Assignment of Ministerial Functions] Notice, 2006), ambalo lilichapishwa katika Gazeti la Serikali kama Tangazo la Serikali Na. 2 la tarehe 13 Januari, 2006. Tangazo hilo lilifuta Matangazo mengine yote ya miaka ya nyuma;
-
Mwaka 2010 Rais Kikwete alitoa Tangazo la Ukasimishaji wa Majukumu ya Kiuwaziri la mwaka 2010 (The Ministers [Assignment of Ministerial Functions] Notice, 2010). Tangazo hilo lilichapishwa katika Gazeti la Serikali kama Tangazo la Serikali Na. 494A la tarehe 17 Disemba, 2010. Kama ilivyokuwa kwa Tangazo la mwaka 2006, Tangazo la 2010 lilifuta Matangazo mengine yote yaliyotolewa kabla ya tarehe 17 Disemba, 2010.
Mheshimiwa Spika,
Katikati ya Matangazo haya, Marais waliomtangulia wa nchi yetu Rais Magufuli, katika vipindi tofauti tofauti, wamekuwa wakitumia mamlaka yao chini ya kifungu cha 5(1) cha Sheria, kufanya marekebisho katika majukumu ya kiuwaziri ambayo yalikuwa chini ya Rais mwenyewe, au aliyakasimisha kwa Mawaziri. Hivyo, kwa mfano, mwaka 1982, Mwalimu Nyerere alitoa Tangazo la Serikali Na. 133 la 1982 kwa ajili hiyo. Mwaka 1984, Mwalimu Nyerere alifanya marekebisho mengine kupitia Tangazo la Serikali Na. 210 la 1984.
Aidha, mwaka 1987, Rais Mwinyi alifanya marekebisho kupitia Tangazo la Serikali Na. 206 la tarehe 17 Aprili, 1987. Mwaka uliofuata, Rais Mwinyi alifanya marekebisho mengine kupitia Tangazo la Serikali Na. 42 la tarehe 26 Februari, 1988. Vile vile, mwaka 2003, Rais Mkapa alitoa Tangazo la Serikali Na. 142 la tarehe 16 Mei, 2003. Mwaka huo huo, Rais Mkapa alifanya marekebisho mengine kupitia Tangazo la Serikali Na. 413 la tarehe 19 Disemba, 2003. Aidha, mwaka uliofuata Rais Mkapa alifanya marekebisho mara mbili kupitia Tangazo la Serikali Na. 79 la tarehe 12 Machi, 2004, na Tangazo la Serikali Na. 523 la tarehe 3 Disemba, 2004.
Mheshimiwa Spika,
Tumeelezea jambo hili kwa kirefu kiasi kwa sababu lina umuhimu mkubwa kikatiba na kisheria. Rais hatakiwi kugawa wizara, idara za serikali na majukumu ya kiuwaziri kiholela. Haya ni majukumu ya umma na, kwa sababu hiyo, ni lazima yafanywe kwa kufuata taratibu za kisheria zilizopo. Kwa upande wao, Mawaziri wanatakiwa kutekeleza majukumu waliyokasimiwa na Rais kwa mujibu wa Sheria ya Utekelezaji wa Majukumu ya Kiuwaziri. Majukumu hayo lazima kwanza yatamkwe, yafafanuliwe na kuainishwa katika Tangazo lililochapishwa kwa ajili hiyo katika Gazeti la Serikali. Ndio maana, kwa mujibu wa kifungu cha 5(1) cha Sheria hiyo, ushahidi pekee na wa mwisho juu ya suala kama Waziri ana mamlaka katika jambo fulani, ni Tangazo la Rais lililochapishwa chini ya kifungu hicho.
Mheshimiwa Spika,
Kwa sababu ambazo Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu inapenda Bunge hili lizifahamu, licha ya mabadiliko makubwa katika, idadi, muundo na majukumu ya Wizara mbali mbali, hadi tunapoandika Maoni haya, Rais Magufuli hajatoa Tangazo lolote juu ya majukumu ya kiuwaziri ambayo yeye mwenyewe amejibakishia na/au yale ambayo ameyakasimu kwa Mawaziri aliowateua. Tofauti na alivyofanya Rais Kikwete na Serikali yake mwaka 2010, hakuna Mbunge hata mmoja ndani ya Ukumbi huu ambaye amepatiwa nakala ya Tangazo lolote lililochapishwa kwa mujibu wa Sheria.
Licha ya madai ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu katika hotuba yake Bungeni ya tarehe 22 Aprili ya mwezi uliopita, Bunge lako tukufu halijapatiwa nakala hata moja inayothibitisha kwamba Mawaziri walioteuliwa na Rais Magufuli, na ambao wamekuwa wakifanya mambo mbali mbali kwa kofia za kiuwaziri, wanatekeleza majukumu waliyokasimishwa kwa mujibu wa Sheria ya Utekelezaji wa Majukumu ya Kiuwaziri.
Ukweli ni kwamba hata Waziri Mkuu, Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa, amekiri kwamba Serikali inaendeshwa bila kuwa na alichokiita ‘instrument.’ Kwa maneno yake mwenyewe, wakati akifanya majumuisho ya hoja za Wabunge kwa Ofisi yake tarehe 27 Aprili, Waziri Mkuu amesema kwamba “instrument za Wizara zote zimeshakamilika na zimesainiwa (tarehe) 20/04; sasa tunasubiri kutangaza, wakati wowote Mheshimiwa Rais atakapoamua kutangaza zitakuwa zimetoka.” Maana ya kauli hii ni kwamba hakuna instrument yoyote iliyotangazwa kama inavyotakiwa na kifungu cha 5(1) cha Sheria.
Mheshimiwa Spika,
Maana na athari ya kisheria ya kutokuwepo kwa Tangazo la ukasimishaji wa majukumu ya kiuwaziri ni kubwa sana. Wengi wa Mawaziri wa Serikali hii waliteuliwa na Rais Magufuli tarehe 10 Disemba, 2015. ‘Viporo’ vilivyobakia kwenye Baraza la Mawaziri vilikamilishwa tarehe 23 Disemba, 2015. Tangu wakati huo hadi sasa, Mawaziri wamefanya mambo mengi. ‘Wametumbua majipu’ katika Wizara zao na taasisi zilizo chini yake kwa kufukuza, kuachisha, kusimamisha kazi au kuhamisha watendaji na watumishi mbali mbali wa Wizara au taasisi hizo. Wamefanya maamuzi juu ya matumizi ya fedha na rasilmali nyingine za umma.
Yote waliyoyafanya wameyafanya kinyume cha sheria. Hawakuwa na mamlaka ya kufanya waliyoyafanya kwa sababu Mawaziri hawa hawajakasimishwa mamlaka ya utekelezaji wa majukumu yao kwa mujibu wa kifungu cha 5(1) cha Sheria ya Utekelezaji wa Majukumu ya Kiuwaziri. Watendaji na watumishi wote ambao wametumbuliwa majipu na mawaziri hawa wana haki na uwezo wa kwenda mahakamani na kuomba Mahakama zetu zitengue utumbuaji wa majipu waliofanyiwa na Mawaziri wasiokuwa na mamlaka hayo kinyume cha Sheria hii.
Ushauri wangu wa bure kwa watendaji na watumishi hao ni kwamba wakafungue mashauri Mahakama Kuu ya Tanzania kupinga kutumbuliwa kwao majipu na watu wanaojiita Mawaziri lakini hawana hata job description! Kwenda kwao mahakamani sio kutawasaidia kupata haki zao, bali pia kutakomesha vitendo vya kuendesha nchi kienyeji enyeji na bila kufuata sheria, vinavyoelekea kushamiri chini ya utawala huu wa Rais John Pombe Magufuli.
Mheshimiwa Spika,
Kila mtu anafahamu kwamba Rais John Pombe Magufuli sio mwanasheria. Hata hivyo, pamoja na kutokuwa mwanasheria, Rais Magufuli naye anatakiwa kufuata sheria za nchi. Hayuko juu ya sheria. Kiapo chake kinamtaka ‘kuilinda, kuitetea na kuihifadhi’ Katiba ya nchi yetu na sheria zake. Aidha, Mamlaka ya Nchi na vyombo vyake vyote vinawajibika, kama inavyotamka ibara ya 9(b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977, “… kuhakikisha … kwamba sheria za nchi zinalindwa na kutekelezwa.”
Kwa sababu Rais Magufuli sio mwanasheria, ameteua Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye – kwa maneno ya ibara ya 59(3) ya Katiba – “ndiye mashauri wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano juu ya mambo ya sheria na … atawajibika kutoa ushauri kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano juu ya mambo yote ya kisheria….” Aidha, kwa sababu hiyo hiyo, Rais Magufuli ameteua Waziri wa Katiba na Sheria ili, kama inavyotakiwa na ibara ya 54(3), awe mshauri wake mkuu katika utekelezaji wa madaraka yake katika masuala ya kikatiba na kisheria.
Kwa bahati nzuri, Rais Magufuli amemteua pia Dkt. Harrison George Mwakyembe – mmoja wa wasomi wa juu kabisa wa sheria katika nchi yetu – kuwa Waziri wake wa Katiba na Sheria. Vile vile, Rais Magufuli amemteua Dkt. Sifuni Ernest Mchome – msomi mwingine wa juu kabisa wa sheria – kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria; na Bwana Amon Anastazi Mpanju, mwanasheria mwingine tena, kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo. Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu inataka kupatiwa majibu sahihi ni kwa nini wanasheria wabobezi wote hawa wameshindwa kumshauri Rais Magufuli kutoa Tangazo la kukasimisha majukumu ya kiuwaziri kwa Mawaziri mbali mbali aliowateua karibu miezi sita iliyopita. Serikali inaendeshwa kama mali binafsi ya Rais Magufuli, bila kufuata wala kuheshimu sheria, sio tu kwa sababu Rais Magufuli ana viashiria vyote vya utawala wa kiimla, bali pia kwa sababu anaelekea kutokuwa na washauri katika masuala ya katiba na sheria za nchi.
Kwa kuangalia mifano ya Matangazo mbali mbali ambayo yametolewa na watangulizi wa Rais Magufuli tangu Sheria ya Utekelezaji wa Majukumu ya Kiuwaziri ilipotungwa mwaka 1980, hata mwanafunzi wa sheria wa mwaka wa kwanza angeweza kumtengenezea Rais Magufuli draft ya Tangazo la aina hiyo. Iweje watu wenye shahada za uzamivu na uzamili katika sheria washindwe kufanya hivyo kwa karibu nusu mwaka tangu wateuliwe? Kama ni majipu ya kutumbuliwa na Rais Magufuli, basi wasomi hawa wa sheria ni majipu na wanastahili kutumbuliwa. Itatushangaza sana endapo Rais Magufuli atayafumbia macho majipu haya.
UCHAGUZI WA ZANZIBAR NA UKOLONI WA TANGANYIKA
Mheshimiwa Spika,
Sasa naomba nizungumzie masuala ya kikatiba yanayohusu Muungano wetu. Kwa wasiofahamu Katiba yetu na wanaoweza kuhoji kwa nini tunazungumzia masuala ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar katika hoja iliyoko mezani, Sura ya Nne yote ya Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano inahusu ‘Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (na Rais wa Zanzibar), Baraza la Mapinduzi la Zanzibar na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.’ Aidha, ibara ya 104 ya Katiba yetu imewekwa mahsusi kwa ajili ya ‘Uchaguzi wa Kiongozi wa Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.’ Kwa sababu hizi, ni halali kabisa kuzungumzia yaliyotokea Zanzibar katika hoja iliyoko mezani.
Mheshimiwa Spika,
Katika Maoni yake juu ya Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Makamu wa Rais kwa Mwaka wa Fedha 2014/2015, Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu – baada ya uchambuzi wa kina wa masuala ya fedha za Muungano – ilisema yafuatayo kuhusu mahusiano kati ya Tanganyika na Zanzibar tangu Muungano wetu uzaliwe tarehe 26 Aprili, 1964:
“Kwa vyovyote vile, takwimu hizi zinaonyesha kwamba, kwa sababu ya Muungano huu, uhusiano kati ya Tanganyika na Zanzibar ni uhusiano wa kinyonyaji. Kwa sababu hiyo, huu ni uhusiano wa kikoloni. Ni uhusiano kati ya ‘himaya’ ya Tanganyika na ‘koloni’ lake la Zanzibar. Himaya za kikoloni huwa zinadhibiti masuala yote ya ulinzi na usalama, mambo ya nje na uhusiano wa kimataifa, uraia, kodi, fedha, sarafu na benki kuu ya makoloni yao. Na himaya za kikoloni huwa zinatumia nguvu na udhibiti wao wa masuala haya kuyanyonya makoloni yao kiuchumi, kuyadidimiza kijamii na kuyatawala kisiasa. Hivi ndivyo ambavyo imekuwa kwa mahuasiano kati ya Tanganyika na Zanzibar tangu kuzaliwa kwa Muungano huu tarehe 26 Aprili, 1964.”
Mheshimiwa Spika,
Tangu mara baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya tarehe 12 Januari, 1964, hadi leo hii, Tanganyika imeidhibiti Zanzibar kijeshi na kisiasa. Ukweli ni kwamba – kama ambavyo Harith Ghassany ameonyesha katika kitabu chake Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru! Zanzibar na Mapinduzi ya Afrabia – Serikali ya Tanganyika ilishiriki kwa kiasi kikubwa katika maandalizi ya Mapinduzi, ikiwemo kutoa silaha na mafunzo ya kijeshi katika mashamba ya mkonge ya Sakura Estates, Pangani, Tanga, kwa walioipindua Serikali ya Waziri Mkuu Mohamed Shamte na Sultan Jamshid bin Abdullah.
Aidha, siku tatu tu baada ya Mapinduzi hayo, Serikali ya Tanganyika – kupitia Waziri wake wa Mambo ya Nje na Ulinzi Oscar Salatiel Kambona – ilipeleka vikosi vya Tanganyika Rifles, Jeshi la Tanganyika, ili kuidhibiti Zanzibar kijeshi. Mambo yote haya yamejulikana kwa miaka mingi na wasomi na wanazuoni wa Muungano huu, na yamechapishwa katika vitabu na machapisho mengine rasmi ya kitaaluma ndani na nje ya Tanzania.
Kwa kutumia udhibiti wake wa kijeshi, Tanganyika imedhibiti pia siasa za Zanzibar. Watawala wa Tanganyika ndio wanaoamua nani awe mtawala wa Zanzibar na wamefanya hivyo tangu mwaka 1964. Alhaj Aboud Jumbe Mwinyi asingekuwa Rais wa Zanzibar baada ya kuuawa kwa Sheikh Abeid Amani Karume mwaka 1972 bila ‘ushawishi’ wa Mwalimu Nyerere na Serikali ya Tanganyika. Na kama ambavyo wanazuoni wa Muungano huu, kama vile Profesa Issa G. Shivji wameonyesha, Jumbe asingeng’olewa madarakani mwaka 1984 bila shinikizo la Mwalimu Nyerere na watu wake hapa Dodoma. Aidha, Rais Mwinyi na Marais wengine wote wa Zanzibar waliomfuatia, ‘wametengenezewa’ Dodoma na sio Zanzibar.
Mheshimiwa Spika,
Tarehe 20 Aprili, 1968, Mwalimu Nyerere alisema yafuatayo wakati akihojiwa na gazeti la The Observer la London, Uingereza: “If the mass of the people of Zanzibar should, without external manipulation, and for some reason of their own, decide that the Union was prejudicial to their existence, I could not bomb them into submission…. The Union would have ceased to exist when the consent of its constituent members was withdrawn.” Yaani, “endapo umma wa wananchi wa Zanzibar wataamua, bila kurubuniwa kutoka nje na kwa sababu zao wenyewe, kwamba Muungano unaathiri kuendelea kuwepo kwao, sitaweza kuwalazimisha kwa kuwapiga mabomu…. Muungano hautaendelea kuwepo pale ridhaa ya washirika wake itakapoondolewa.”
Alichokisema Baba wa Taifa kwamba hatakifanya, Serikali ya Tanganyika imekifanya kwa zaidi ya miaka ishirini sasa. Kabla ya mfumo wa vyama vingi kuruhusiwa mwaka 1992, udhibiti wa Tanganyika kwa siasa za Zanzibar ulifanyika kwa kutumia dhana ya ‘chama kushika hatamu.’ Katika zama za vyama vingi, wananchi wa Zanzibar wamekuwa wapinzani wakubwa wa ukoloni wa Tanganyika kwa nchi yao. Kwa sababu hiyo, tangu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995, Serikali ya Tanganyika imetumia mabavu ya kijeshi ya wazi wazi ili kuwaweka madarakani vibaraka wake na kuendelea kuitawala Zanzibar.
Kilele cha matumizi haya ya mabavu ya kijeshi ni Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, ambako vibaraka wa Tanganyika katika Zanzibar walikataliwa kabisa na wananchi wa Zanzibar katika Uchaguzi wa Rais, Wawakilishi na Madiwani. Ni Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) tu ndilo ambalo limehakikisha kwamba vibaraka hawa waliokataliwa na wananchi wao, wanaendelea kubakia madarakani.
Kwa maoni yetu, Mheshimiwa Spika, katika mazingira haya, tatizo la msingi la Zanzibar sio Jecha Salim Jecha wala ZEC wala Ali Mohamed Shein. Hawa ni vibaraka tu wasiokuwa na nguvu wala uhalali wowote. Bila nguvu ya Tanganyika vibaraka hawa hawawezi kudumu madarakani kwa muda mrefu. Tatizo la msingi ni ukoloni wa Tanganyika kwa Zanzibar ambao umevikwa joho la Muungano. Bila kulivua joho hili na kushona lingine badala yake, Zanzibar haitakuwa huru na itaendelea kutawaliwa na Tanganyika kisiasa, kiuchumi na kijeshi.
KUNYAMAZISHA UPINZANI NI KUKARIBISHA UDIKTETA!
Mheshimiwa Spika,
Mwanaharakati mmoja wa haki za binadamu wa karne ya 19 aliwahi kuandika kwamba: “Once a government is committed to the principle of silencing the opposition, it has only one way to go, and that is down the path of increasingly repressive measures, until it becomes a source of terror to all its citizens and creates a country where everyone lives in fear”, yaani “pale serikali inapoamua kunyamazisha upinzani, inakuwa na njia moja tu ya kupita, nayo ni njia ya kuongezeka kwa vitendo vya kikandamizaji, mpaka serikali hiyo inakuwa chanzo cha hofu kwa wananchi wake wote na inatengeneza nchi ambapo kila mmoja anaishi kwa hofu.”
Maneno haya yametimia katika nchi yetu. Kwa sababu ya kubaka demokrasia kwa kutumia nguvu za kijeshi Zanzibar ili kukipokonya Chama cha Wananchi (CUF) ushindi wake halali, Serikali hii ya hapa kazi tu imeingia katika njia ya kuongezeka kwa vitendo vya kikandamizaji kila mahali katika nchi yetu. Katika Jiji la Tanga ambako CCM ilikataliwa na wananchi, Serikali hii ilitumia ghilba na mabavu ya kila aina kuhakikisha CCM inanyakua Umeya wa Jiji hilo. Leo viongozi wa vyama vya UKAWA na madiwani waliochaguliwa na wananchi wanakabiliwa na mashtaka ya kutengeneza kwa sababu tu ya kukataa kwao kutawaliwa na watu ambao hawakupata ridhaa ya wananchi.
Hivyo ndivyo ilivyotokea katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero, ambako ilibidi Mbunge wa Jimbo la Kilombero na mjumbe halali wa Halmashauri hiyo atolewe kwa nguvu na mapolisi ili kuiwezesha CCM, iliyokataliwa na wananchi kwenye kura, kushinda nafasi ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya. Sasa Mbunge huyo naye anakabiliwa na mashtaka ya jinai mahakamani kwa kosa la kutetea demokrasia na utawala wa sheria na kukataa utawala wa mabavu na udikteta.
Katika Jiji la Dar es Salaam na Halmashauri zake, licha ya nguvu kubwa na hila nyingi zilizotumiwa na Serikali hii, wananchi wa Dar es Salaam na viongozi wao wa UKAWA walifanikiwa kutetea maamuzi ya wapiga kura na kuzuia jaribio la kubaka demokrasia kwa kuweka Mameya wa chama kilichokataliwa na wananchi kwenye uchaguzi. Hata hivyo, badala ya kuchukua hatua za kijinai dhidi ya Mkurugenzi wa Jiji, Mwanasheria wa Jiji na Katibu Tawala wa Mkoa waliodiriki hata kugushi hati ya amri ya Mahakama kwa lengo la kuzuia uchaguzi halali wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, leo wanaokabiliwa na mashtaka ya jinai ni Wabunge Halima James Mdee, Saed Ahmed Kubenea na Mwita Mwikwabe Waitara waliohakikisha kwamba uhuni huu wa kisiasa haufanikiwi katika Jiji la Dar es Salaam.
Na sio vyama vya siasa na wanasiasa tu ambao wameangukiwa na adha hii ya Serikali kuingia katika njia ya ukandamizaji. Kwa sababu Rais anatumbua majipu hadharani na, hasa, kwenye vyombo vya habari, sasa Mawaziri nao wanatumbua majipu ya Wizara zao hadharani. Haijalishi kwamba Waziri hawa sio mamlaka ya kinidhamu ya utumishi wa umma na, kama tulivyoonyesha, wala hawajakasimishwa majukumu yoyote kisheria, sasa Mawaziri wanafukuza au kusimamisha au kuhamisha watumishi wa umma walio chini yao.
Wakuu wa Mikoa nao sasa wanatumbua majipu mikoani; wanasimamisha Wakurugenzi wa Halmashauri za Serikali za Mitaa na watumishi wengine wa serikali za mitaa bila kujali kwamba hawana mamlaka yoyote kisheria ya kufanya hivyo. Na siku hizi haipiti wiki moja bila kusikia kwenye vyombo vya habari kwamba Mkuu wa Mkoa au Wilaya fulani ameamuru ameamuru afisa huyu ama yule wa Halmashauri, au diwani huyu au yule, akamatwe kwa sababu hii au ile.
Wote hawa wanafanya hivyo ili wajionyeshe kwamba wanafanya kazi ya Bwana Mkubwa ili asije akawatumbua majipu wao wenyewe. Hofu ya kutumbuliwa majipu ama na Rais mwenyewe ama na Mawaziri ama na Wakuu wake wa Mikoa na Wilaya wake sasa imetanda kila mahali katika utumishi wa umma. Hofu hii inatokana na ukweli kwamba katika kutumbua majipu huku, hakuna tena kufuata utaratibu wa kinidhamu uliowekwa na sheria za nchi yetu. Sasa hatua hizo zinachukuliwa na wasio na mamlaka kisheria katika majukwaa ya kisiasa au kwenye mikutano ya waandishi habari. Na hakuna aliye salama, kuanzia Katibu Mkuu Kiongozi hadi nesi wa hospitalini na mfagizi wa ofisini. Nchi yetu imeingia katika mteremko wenye utelezi mwingi kuelekea kwenye dola la kidikteta.
Mheshimiwa Spika,
Kwa vile Serikali hii ya Rais Magufuli imekumbatia dhana ya kunyamazisha upinzani dhidi yake, uhuru wa vyombo vya habari umewekwa rehani. Kwa kuwa Bunge hili lilijitokeza, katika miaka kumi ya utawala wa Rais Kikwete, kama chombo chenye nguvu ya kuiwajibisha Serikali na watendaji wake, Serikali ya hapa kazi tu imeamua kulinyamazisha na kulifanya kama lilivyokuwa wakati wa miaka ya ‘chama kushika hatamu’, yaani chombo cha kupiga muhuri na kuhalalisha maamuzi ya watawala.
Wala sio siri tena kwamba Kamati za Kudumu za Bunge hili zimepangiwa nje ya Bunge na mamlaka ambazo sio za kikatiba wala kikanuni. Na wala sio siri tena kwamba sasa Bunge hili linaongozwa kwa maagizo ya Ikulu. Ndio maana kila kiongozi wa Bunge sasa anajipendekeza Ikulu kwa vitendo ambavyo mara nyingine vinafedhehesha, kama vile kumpelekea Rais Magufuli fedha zilizoidhinishwa na Bunge hili kwa ajili ya matumizi yake ili zikanunue madawati ya mashule. Kufuta matangazo ya moja kwa moja ya televisheni ni sehemu tu ya mkakati wa kulinyamazisha Bunge ili lisiendelee kuwa chombo cha kuiwajibisha Serikali.
Mkakati wenyewe ni kunyamazisha upinzani dhidi ya utawala huu. Mkakati huu umelenga vile vile kunyamazisha vyombo binafsi vya habari ambavyo wakati mwingine vimekuwa ni sauti ya upinzani kwa watawala wa nchi hii. Ndio maana hata nusu mwaka haikupita na Serikali hii ikaanza kufuta – sio kufungia! – magazeti binafsi yanayotoa habari zisizowapendeza watawala, na kutishia hatua hiyo hiyo kwa magazeti mengine.
Mheshimiwa Spika,
Hata Mahakama ya Tanzania haijapona wimbi hili la ‘kuongezeka kwa vitendo vya kikandamizaji.’ Ibara ya 107A(1) ya Katiba ya nchi yetu inatamka wazi kwamba “mamlaka yenye kauli ya mwisho ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano itakuwa ni Mahakama.” Aidha, ibara ya 107B ya Katiba hiyo imeweka wazi kwamba “katika kutekeleza mamlaka ya utoaji haki, mahakama zote zitakuwa huru na zitalazimika kuzingatia tu masharti ya Katiba na yale ya sheria za nchi.”
Licha ya msimamo huu wa kikatiba, Serikali hii ya hapa kazi tu imeanza kuingilia uhuru wa mahakama kwa njia za ajabu, kama sio za kutisha. Kwa mfano, wakati wa sherehe za ufunguzi wa mwaka wa kimahakama mwanzoni mwa mwezi Februari ya mwaka huu, Rais wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS), Bwana Charles Rwechungura alitoa mfano wa Mkuu wa Wilaya ya Babati, Crispin TP Meela (mwenyewe mwanasheria na mwanachama wa TLS!) aliyeamuru hakimu mmoja wa Mahakama ya Mwanzo akamatwe na kuwekwa mahabusu baada ya hakimu huyo kutoa hukumu ambayo haikumfurahisha Mkuu wa Wilaya.
Kitendo kama hicho kiliwahi kutokea katika miaka ya 1970 wakati Mkuu wa Mkoa wa Mara alipoamuru watuhumiwa waliopewa dhamana na Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Musoma wakamatwe na kurudishwa rumande. Hakimu Mkazi aliyewapa watuhumiwa hao dhamana alichukua hatua ya kumjulisha Jaji Mkuu, wakati huo Marehemu Francis Lucas Nyalali juu ya kitendo hicho cha Mkuu wa Mkoa. Siku hiyo hiyo taarifa hizo zilimfikia Rais Nyerere na wiki mbili baadae Mkuu wa Mkoa alihamishwa kutoka Mkoa wa Mara. Leo hakimu anakamatwa kwa amri ya Mkuu wa Wilaya lakini kwa sababu ya hofu iliyotanda ya kutumbuliwa majipu, Jaji Mkuu na Mahakama nzima imenyamaza kimya.
MAJIPU YA MAHAKAMA!
Mheshimiwa Spika,
Sasa naomba nizungumzie masuala ya Mahakama ya Tanzania ambayo, kwa sababu ya utamaduni uliojengeka kwa miaka mingi wa kulindana, hayazungumzwi. Tarehe 30 Novemba, 2014, Bunge hili lilipitisha kwa kauli moja Maazimio ya Bunge Kuhusu Hoja ya Taarifa Maalum ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali Kuhusu Taarifa ya Ukaguzi Maalum Kuhusiana na Miamala Iliyofanyika Katika Akaunti ya ‘Escrow’ ya Tegeta Pamoja na Umiliki wa Kampuni ya IPTL, maarufu kama Maazimio ya Tegeta Escrow Account.
Azimio la 4 la Maazimio ya Tegeta Escrow Escrow lilisema yafuatayo: “KWA KUWA, Taarifa Maalum ya Kamati imeonesha kwamba katika watu waliotajwa kuhusika kwa namna moja au nyingine katika kashfa ya miamala ya Akaunti ya Escrow wapo pia Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania; KWA KUWA, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 … imeweka utaratibu mahsusi wa kushughulikia nidhamu ya Majaji; KWA KUWA, utaratibu wa kushughulikia nidhamu ya Majaji kwa mujibu wa Katiba unamtaka Rais kuunda Tume ya Uchunguzi wa Kijaji kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya Majaji; NA KWA KUWA, utaratibu wa kushughulikia nidhamu ya Majaji unamruhusu Rais kumsimamisha kazi Jaji au Majaji husika wakati uchunguzi wa tuhuma dhidi yake unaendelea; HIVYO BASI, BUNGE LINAAZIMIA KWAMBA, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aunde Tume ya Kijaji ya Uchunguzi kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya Jaji Aloysius Mujulizi na Jaji Profesa Eudes Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya Tanzania.”
Mheshimiwa Spika,
Baada ya Bunge lako tukufu kupitisha maazimio haya, tarehe 22 Disemba, 2014, Rais Jakaya Kikwete aliwahutubia ‘Wazee wa Dar es Salaam’ ambako alisema yafuatayo kuhusu Azimio la Majaji wa Tegeta Escrow: “Azimio hili nimelipokea, (na) tumelijadili. Hata hivyo, itabidi tufuate utaratibu wa kikatiba na kisheria wa kushughulikia masuala ya namna hiyo. Inatakiwa suala kama hili lianzie kwenye Mhimili wa Mahakama yenyewe na siyo kwa Rais au Bunge. Tume ya (Utumishi wa) Mahakama ndiyo yenye mamlaka ya kumtaka Rais aunde Tume ya Kijaji ya kumchukulia hatua Jaji yeyote pale inapodhihirika kuwa amepoteza sifa za kuendelea kufanya kazi hiyo. Nashauri suala hili tumuachie Jaji Mkuu wa Tanzania alishughulikie atakavyoona inafaa.”
Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa na vyombo vya habari mwaka jana, baada ya maelezo hayo ya Rais Kikwete, Jaji Mkuu, Mheshimiwa Mohamed Chande Othman aliunda jopo la Majaji watatu, chini ya Mwenyekiti wake, Jaji Mbarouk Salim Mbarouk wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania. Aidha, mwishoni mwa mwaka jana, Jaji Mkuu Othman aliwaambia waandishi habari kuwa taarifa ya uchunguzi ya Tume ya Jaji Mbarouk ilikuwa ‘imeiva.’ Cha kushangaza, Mheshimiwa Spika, tangu kuiva kwa taarifa hiyo, Jaji Mkuu Othman, na Serikali hii ya CCM, wamepata kigugumizi kikubwa cha ‘kuipakua’ ili Bunge lako tukufu na Watanzania kwa ujumla ‘waile’! Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu inamtaka mtoa hoja alieleze Bunge lako tukufu iliko taarifa ya uchunguzi wa Majaji wa Tegeta Escrow na kwa nini haijaletwa mbele ya Bunge lako tukufu kwa taarifa au kwa mjadala.
SOMO KUTOKA KENYA
Mheshimiwa Spika,
Hatuna budi kujifunza namna ya kushughulikia masuala ya maadili ya Majaji wetu kutoka kwa jirani zetu. Naomba, katika hili, kutoa mfano wa hivi karibuni kutoka nchini Kenya. Mapema mwaka huu, Jaji Phillip Tunoi wa Mahakama ya Juu (Supreme Court) ya Kenya alituhumiwa katika kashfa inayofanana na kashfa ya Majaji wa Tegeta Escrow. Mara baada ya tuhuma dhidi ya Jaji Tunoi kutolewa hadharani, Jaji Mkuu wa Kenya, Dkt. Willy Mutunga, aliunda Tume ya Uchunguzi ya Kijaji kuchunguza tuhuma hizo. Mnamo tarehe 5 Februari ya mwaka huu, ndani ya kipindi cha wiki mbili, Jaji Mkuu Mutunga alimkabidhi Rais Uhuru Kenyatta taarifa ya uchunguzi wa tuhuma dhidi ya Jaji Tunoi. Kwetu Tanzania ni zaidi ya mwaka na nusu tangu Bunge lako tukufu lipitishe azimio la kuunda Tume ya kuwachunguza Majaji wa Tegeta Escrow na Jaji Mkuu wetu anaelekea kuwa amekalia taarifa ya uchunguzi huo, kama kweli ulifanyika.
Tarehe 12 Februari, 2016, Kamati ya Kudumu ya Fedha za Serikali (PAC) ya Bunge la Kenya ilitoa taarifa iliyomtuhumu Jaji Mkuu Mutunga kuwa hachukui hatua zozote dhidi ya vitendo vya rushwa vinavyofanywa na Majaji, Wasajili na Mahakimu wa Kenya. PAC ya Kenya ilimtaka Jaji Mkuu Mutunga kuwajibika ama kuwajibishwa, ikiwa ni pamoja na kuondolewa kwenye nafasi ya Jaji Mkuu wa Kenya kwa kushindwa kudhibiti maadili ya maafisa hao wa Mahakama ya Kenya.
Siku moja baadae, Jaji Mkuu Mutunga aliijibu PAC kwa kutoa takwimu zilizothibitisha jitihada za Mahakama ya Kenya katika kukabiliana na rushwa na ufisadi ndani ya Mahakama hiyo. Kwa maelezo ya Jaji Mkuu Mutunga, “… three judges have been referred to a tribunal … on allegations of corruption, a few others are under consideration in the Judicial Service Commission, a Chief Registrar and five Directors have been dismissed, 9 magistrates and 65 Judicial Staff are facing disciplinary proceedings, some have been dismissed or retired in the public interests….”
Kwetu Tanzania, kwa mujibu wa Taarifa ya Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Harrison G. Mwakyembe (MB), Akiwasilisha Mpango na Makadirio ya Bajeti ya Wizara Kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 mwezi uliopita: “Tume (ya Utumishi wa Mahakama) ilishughulikia jumla ya mashauri 14 ya nidhamu kwa watumishi wa mahakama na kutolewa uamuzi. Katika hayo watumishi 10 walifukuzwa kazi baada ya kupatikana na hatia ya utovu wa nidhamu na mengine 4 yanafanyiwa uchunguzi zaidi.”
Na kwa kadri ya ufahamu wa Kambi Rasmi ya Upinzani ya Bunge lako tukufu, mara ya mwisho Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania aliwahi kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa utovu wa maadili ilikuwa ni mwanzoni kabisa mwa miaka ya 1990, wakati Jaji Mwakibete alipoondolewa na Rais Ali Hassan Mwinyi kwa tuhuma za rushwa na baada ya kuundiwa Tume ya Uchunguzi ya Kijaji. Tangu wakati huo, inaelekea Majaji wa Tanzania wamekuwa malaika na watakatifu wasiokula kula rushwa wala kufanya makosa mengine ya utovu wa maadili, maana hakuna hata mmoja ambaye ameundiwa Tume ya Uchunguzi ya Kijaji au kuchukuliwa hatua stahiki za kinidhamu.
Hii, Mheshimiwa Spika, haiwezi kuwa kweli. Kwa jinsi ambavyo tuhuma za rushwa na ufisadi katika ngazi zote za Mahakama ya Tanzania zimekuwa kubwa na kwa miaka mingi, ni wazi hatuna malaika wala watakatifu katika Mahakama ya Tanzania. Na kwa ushahidi wa Addendum Juu ya Uteuzi wa Majaji niliyoitoa kufuatia Maoni yangu mbele ya Bunge lako tukufu ya tarehe 13 Julai, 2012, matatizo ya utovu wa maadili katika Mahakama zetu za juu ni makubwa sana.
Kwa sababu hiyo, ni lazima sisi kama Bunge na kama taifa tutumbue majibu makubwa na mengi ya Mahakama ya Tanzania. Bunge lako tukufu lisinyamaze kwa hofu ya kuwaudhi Majaji na Mahakimu wetu. Kukosekana kwa haki katika Mahakama zetu kutapelekea machafuko katika nchi yetu. Kama kiongozi maarufu wa Mapinduzi ya Mexico ya 1910, Emiliano Zapata, alivyowahi kusema: “If there is no justice for the people, let there be no peace for the government”, yaani “kama hakuna haki kwa wananchi, basi kusiwe na amani kwa serikali.”
Tundu Antiphas Mughwai Lissu
MSEMAJI & WAZIRI KIVULI, WIZARA YA KATIBA NA SHERIA
MEI 5, 2016
Filed under: Siasa Tagged: Karume, Lissu, Muungano, Nyerere, Tanzania, Zanzibar

Vituko vya bajeti ya SMZ
Nimeipitia bajeti ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na kugundua kuwa haitekelezeki na kiini macho cha kiwango cha shahada ya uzamifu (PhD). Kwa haraka haraka nimebaini masuala yafuatayo:
Kwanza, bajeti ya jumla iliyotangazwa ni shilingi bilioni 841.5 kwa mwaka wa fedha 2016/2017. Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 445.6 zitatumika kwa matumizi ya kawaida (chai, mishahara n.k.) na shilingi bilioni 395.9 zitatumika kwa kazi za maendeleo.
Pili, vyanzo vya mapato vya bajeti hiyo ni Mamlaka ya Mapato ya Tanzania (TRA) kukusanya shilingi bilioni 188.8, wakati Bodi ya Mapato ya Zanzibar (ZRB) itakusanya shilingi bilioni 237.4. Kwa hiyo, jumla Wazanzibari mtakusanya shilingi bilioni 426.2 ambayo ni chini ya nusu ya bajeti nzima mliyopitishiwa.

Tatu, mambo kadhaa ambayo yangeliongeza “vimakusanyo” huku na kule yamefutwa, nadhani, kwa lengo la kulinda uhalali wa watawala. Ambapo mshahara wa kima cha chini umepandishwa kutoka shilingi 150, 000 hadi 300,000, kodi ya mishahara ya wafanyakazi wa kipato cha chini imepunguzwa kutoka asilimia 13 hadi 9 (kama alivyofanya Rais John Magufuli huku Bara) na ongezeko la kodi “kwa lengo la kupunguza mzigo kwa wananchi” limezuiwa.
Nne, Waziri wa Fedha wa Zanzibar, Dk.Khalid Salum Mohamed, anasema bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwamo kupungua kwa fedha kutoka kwa washirika wa maendeleo; na ndiyo maana bajeti hiyo itajikita zaidi katika kuweka kipaumbele cha makusanyo ya kodi ya ndani.
Sasa maoni yangu ni haya yafuatayo:
Kwanza, bajeti ya matumizi ya kawaida ni kubwa zaidi kuliko ile ya maendeleo.
Pili, bajeti haioneshi ni namna gani itaziba pengo la shilingi bilioni takribani 400 ambazo hazitakusanywa na ZRB wala TRA.
Tatu, bajeti haioneshi ni nchi gani wahisani zitaisaidia bajeti ya Zanzibar ya mwaka huu na waziri anakiri wazi kuwa wahisani wamechanja mbuga.
Nne, bajeti inaweka mkazo kwenye makusanyo ya ndani baada ya wafadhili kukataa kuisaidia Zanzibar, bila kukumbuka kuwa makusanyo ya ndani – na hasa biashara za bandari – zimeshayumba na zinatarajiwa kuyumba zaidi mwaka huu. Sijui hao ZRB na TRA watafikiaje malengo ya ukusanyaji ili walau watekeleze hata nusu ya bajeti iliyopitishwa.
Tano, katika utekelezaji wa bajeti zilizopita, TRA na ZRB walikusanya viwango vya chini kuliko vinavyotarajiwa na ndivyo itakuwa pia mwaka huu.
Sita, chini ya utawala wa CCM, Zanzibar imeshindwa kujijengea uchumi wake, Wazanzibari mumeendelea kutegemea misaada ya wahisani, fedha kutoka Tanzania Bara na kadhalika. Mumeachwa kabisa kiuchumi na visiwa mkakati (strategic islands) vilivyotapakaa kote duniani na bajeti hii inaendelea kudhihirisha kuwa bado munahitaji utawala kutoka Tanganyika, nami nadhani watawala wako tayari kuendeleza hila zao juu yenu.
Nimalizie kama nilivyoanza: bajeti hii ni changa la macho la kiwango cha PhD. Jipangeni upya na kujifunga mikanda hasa, maana mutapita kwenye wakati mgumu sana miaka hii michache, siyo kisiasa tu, bali pia na kiuchumi.
Niwatanabahishe jambo moja: Mzee Joseph Sinde Warioba (Waziri Mkuu Mstaafu, Mwana CCM, Mtanganyika), Mzee Salim Ahmed Salim (Kiongozi Mwandamizi wa CCM, Katibu Mkuu Mstaafu wa Umoja wa Mataifa ya Afrika, Mzanzibari) na raia wengine waandamizi wa taifa hili (Wazanzibari + Watanganyika = Watanzania) walikuleteeni Katiba Mpya ambayo ingetoa fursa kubwa kwa Zanzibar kujiamulia masuala yake ya kisiasa na kiuchumi.
Walioongoza kumnafiki na kumtukana Jaji Warioba na kina Dk. Salim ni wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kutoka Zanzibar, wana-CCM kindakindaki. Mukaikataa Zanzibar itakayowafanya mjiamulie masuala yenu wenyewe.
Sasa endeleeni kusubiri shilingi bilioni 100 za TRA kwa sababu mnasubiri mletewe, nasi tutaendelea kuwakusanyia na kuwaletea mapato yenu huko huko. Tusubirieni.
Kidumu Chama Cha Mapinduzi.
Filed under: Siasa Tagged: bajeti, CCM, Dk. Shein, SMZ, Zanzibar

TUNDU LISSU: Mpambanaji aliyeuanza uwanaharakati utotoni
JUNI 3, mwaka huu, Mwandishi Wetu, Godfrey Dilunga, alifanya mahojiano kuhusu masuala mbalimbali na Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA) ambaye pia ni mwanaharakati wa haki za binadamu, Tundu Lissu, jijini Dar es Salaam. Yafuatayo ndiyo yaliyojiri kwenye mahojiano hayo.
Raia Mwema: Tuanze na historia yako kwa muhtasari.
Lissu: Niliishi maisha ya furaha sana ya utoto. Tangu nikiwa shule ya msingi ni kama vile nilikuwa mwanaharakati. Unajua shuleni kuna shughuli nyingi sana kama kuchota maji kwa ajili ya walimu, kulima mashamba ya walimu na kupanda. Nilikuwa nikiona haya mambo hayako sawa, lakini pia kuna suala la kuwahi shuleni.
Sikumbuki kwa miaka saba ya shule ya msingi, kama kuna siku nimewahi zile namba. Siku zote nilikuwa mchelewaji na nimechapwa kweli.
Raia Mwema: Ni ukaidi wa makusudi?
Lissu: Siwezi kusema ni makusudi, lakini tatizo ni kuamka alfajiri saa 11 ili saa 12 niwe shuleni. Kwa hilo nilikuwa rebel (muasi). Pia sikumbuki mahali ambako sikuwahi kubishana na walimu iwe primary school, secondary school, iwe chuo kikuu, siku zote imekuwa hivyo.
Lakini vile vile nilizaliwa katika familia ambayo mijadala ya kisiasa ilikuwa sehemu yetu. Baba yangu alisoma hadi darasa la sita, mama yangu hakusoma kabisa.
Kila jioni tunasikiliza kwanza taarifa ya habari na idhaa ya Kiswahili ya Ujerumani; baada ya hapo ni mjadala mpaka saa tano au sita, mjadala wa kisiasa kuhusu mwenendo wa mambo duniani. Nilikuwa mtoto mdogo sana, lakini nilikuwa na ufahamu.
Nafikiri nilikuwa miaka sita au saba hivi.
Wakati nikiwa darasa la kwanza (1976), nilikuwa nafahamu karibu viongozi wote duniani na miji mikuu mashuhuri.
Raia Mwema: Kutokana na ufahamu huo, ni viongozi gani hapa nchini walikuvutia wakati huo?
Lissu: Ni swali gumu kidogo. Si rahisi sana kusema nilivutiwa na Mwalimu Nyerere. Ukweli ni kwamba hapana, alikuwa sehemu ya mazungumzo ya kisiasa nchini. Siwezi nikasema nilivutiwa sana na Mwalimu.
Raia Mwema: Unaposikia jina la Julius Nyerere kwa sasa, unakumbuka nini?
Lissu: Ni hotuba za Mwalimu Nyerere kuhusu vita dhidi ya Uganda. Wakati huo nikiwa darasa la tatu mwaka 1978, nchi iko vitani tulichangishwa (familia) ng’ombe.
Baba yangu alitoa ng’ombe watatu kama sikosei ili kusaidia vita mpakani. Shuleni tuliimbishwa sana nyimbo kwamba Iddi Amini ni nyoka; ingawa baadaye nimekuja kugundua kwamba inawezekana kuna vitu vingine vingi hatukuambiwa kuhusu mgogoro wetu na Uganda.
Nakumbuka pia wakati huo tukiwa wadogo tulichimbishwa mahandaki. Nilikuwa na miaka 10, nilishangaa tunachimba (mahandaki) nje ya nyumba yetu halafu siyo marefu sana.
Lakini kuna kitu kingine kilichotafsiri mtazamo wangu kuhusu serikali ambao sio chanya sana. Nilipokuwa miaka kama sita hivi, nyumba yetu na wanavijiji wengine zilibomolewa halafu tukaachwa tu. Kina mama wanalia, kila mtu analia; halafu hawa watu wakavunja nyumba wakaondoka.
Raia Mwema: Hao wavunjaji walitumwa na nani?
Lissu: Unajua ukiwa na miaka 10 huulizi sana. Ni tukio ambalo haliwezi kuondoka katika kumbukumbu zangu kwamba; serikali inaweza kufanya vitu visivyo na akili (mantiki).
Sisi na wanakijiji wengine tumejenga nyumba, ingawa pengine hazikuwa nzuri sana wao (serikali) wametubomolea kwa jina la Operesheni Vijiji.
Baba yangu alikuwa Mwenyekiti wa Kijiji wakati huo, baadaye (watendaji wa serikali) wakaja na kamba za katani na wataalamu ili kupima namna ya kujenga nyumba za kisasa, wanaita maendeleo.
Kwa hiyo, wazee wanatembea na kamba ya katani wanapima namna ya kujenga nyumba za kisasa , zijengwe kwa mstari ulionyooka. Lakini hatimaye hawakutujengea wala kutusaidia chochote.
Hali hiyo ilinifanya niamini kwamba pengine serikali haina watu wenye akili sana kama nilivyokuwa nikifirikia mwanzoni.
Raia Mwema: Ukiwa katika umri wa utoto, unakumbuka nini enzi za nchi kufunga mikanda na baa la njaa lililowahi kutokea?
Lissu: Kuna njaa ya mwaka 1974 serikali ilileta chakula kudhibiti njaa hiyo, nakumbuka kuna kitu (chakula) kinaitwa burga ilikuwa sijaanza shule baadaye tukaletewa ugali wa muhogo. Sisi kwetu tunakula muhogo wa kuchemsha. Ilikuwa hali tofauti.
Raia Mwema: Tueleze safari yako kielimu, ilikuwaje…ngumu au nyepesi tu.
Lissu: Wakati wa Operesheni Vijiji ilitokea mvutano wa kuhama. Baba yangu pamoja na wazee wengine walisafiri kutoka kijijini Singida wakaja Dar es Salaam kulalamika.
Walilalamika kwamba tunatakiwa tuhame kwenye kijiji chenye mashamba makubwa. Wakaja kupiga kelele na serikali wakati huo iliwasilikiza.
Lakini ikaibuliwa hoja kwamba; tuhame (kijiji) kwa sababu hakuna shule. Wakati ule, hoja ya vijiji vya ujamaa ililazimisha kuwapo huduma za kijamii.
Sasa ili kukabili hoja hiyo na tusiweze kuhamishwa, kuna mzee mmoja alijenga nyumba yake mpya, akasema sitahamia ili iwe shule ya watoto. Kwa hiyo, tukaanza shule lakini shida walimu.
Mmoja wa wadogo zake baba yangu wakati huo alikuwa amemaliza darasa la saba, hana pa kwenda, wakasema atakuwa mwalimu. Kuna mama mwingine mjanja mjanja kijijini, naye wakamwambia atakuwa mwalimu.
Kwa hiyo, tukaanza darasa la kwanza Aprili 5, 1976. Shule za miaka ile zilikuwa zinaanza Januari, lakini ya kwetu tulianza Aprili, kwenye nyumba ya tembe sio ya bati, na walimu wasio na mafunzo yoyote.
Hatukuwa na vitabu, swali likawa tutaandikia nini? Wazee wakachanga hela wakamtuma mtu Dar es Salaam aende kumtafuta mtu anaitwa Abdallah Nungu, amueleze tatizo la vitabu shuleni.
Kwa hiyo, tukamsuburi kwa wiki mbili huyu bwana alete vitabu. Akarudi na boski kubwa la vitabu na vile vibao vya kuandikia, ingawa awali tulikuwa tukiandika chini (ardhini). Hivyo ndivyo tulivyoanza shule wengine.
Lakini hilo lilikuwa darasa la kwanza kwenye hiyo nyumba ya mzee. Tatizo likajitokeza ni darasa la pili litakaa wapi, kwa sababu ilibidi darasa la kwanza wengine waanze.
Nyumbani kwetu baba alijenga nyumba jirani na mdogo wake, lakini huyo mdogo wake hakuwa akiishi hapo kijijini alikuwa Moshi, nyumba yake haikuwa ikikaliwa.
Mzee akasema darasa la pili hilo hapo (nyumba ya mdogo wake). Kwa hiyo, darasa la pili tukahamia kwetu (nyumbani). Natoka mlango huu, naingia mlango wa pili niko darasani. Baada ya hapo, tukaanza ujenzi wa shule ambayo ikaitwa Shule ya Msingi Mahambe.
Raia Mwema: Serikali haikutoa mchango wowote katika hatua za awali za ujenzi?
Lissu: Hatukusaidiwa na serikali katika ujenzi. Ilikuwa asubuhi tunakwenda shule, saa nane tunaporudi (shule) tunabeba vibuyu na ndoo za maji pamoja na mama zetu kupeleka eneo la kufyatulia matofali; shughuli iliyokuwa ikifanywa na baba zetu.
Mwaka mzima tumefyatua matofali na baadaye kuanza ujenzi. Kule kwetu kuna Wakatoliki wengi, pale eneo la ujenzi (wa shule) kulikuwa na padre anapita kwenda kusalisha kijiji cha jirani kila Jumatano. Kila akipita anakuta ujenzi unaendelea na watoto wanasaidia.
Huyo padre anaitwa Charles ni mu-Irish, kila siku anapita pale anakuta watoto na wazazi wanafanya kazi, nadhani alikuwa akijiuliza kuna nini?
Siku hiyo akasimama. Alikuwa anatumia pikipiki kubwa….sijui ni kubwa (pikipiki) kweli au mimi ndiye nilikuwa mtoto na kuiona kubwa.
Akauliza, akaambiwa tunajenga shule. Akauliza serikali iko wapi? Akaahidi tukishamaliza ujenzi, ataleta mafundi kukamilisha kwa kuweka bati, ikaitwa Shule ya Wazazi.
Darasa la tatu tukaingia sasa kwenye darasa zuri na bora. Kuanzia hapo, kila mwaka nilipokaa pale shule ya msingi tulikuwa tunajenga darasa moja moja, hadi tulipomaliza mwaka 1979 tunaingia darasa la tano ndiyo kwa mara ya kwanza ikaitwa Shule ya Msingi Mahambe, na tutakaletewa mwalimu wa serikali.
Kwa hiyo, kati ya vyuo vikuu vyangu, chuo kikuu cha kwanza ni hicho….miaka minne ya kufundishwa na walimu wasio na mafunzo yoyote.
Siku hizi nikipita nikiwaambia watu shule niliyosomea na walimu walionifundisha, hawaamini. Tulifundishwa na wanakijiji kabisa wasio na mafunzo! Serikali ilipoanzisha mpango wa UPE wale walimu walijiendeleza, wakaenda vyuoni na wapo ambao wamekuwa waalimu wanataaluma.
Raia Mwema: Hayo ni ya shule ya msingi, tueleze ya sekondari, unakumbuka nini hasa?
Lissu: Cha kwanza nimetoka nje ya kwetu (Singida), nimeenda kusomea Ilboru Sekondari, Arusha. Pale (Ilboru) maisha yalikuwa mazuri na nilikuwa mdogo kuliko wengine wote (wanafunzi).
Sikuwahi kuwa kiongozi shuleni, na sikutaka uongozi. Viongozi wakati ule tuliwaita manyoka kwa sababu wanapeleka habari kwa walimu.
Lakini baadaye nilipoingia kidato cha tano na sita, Galanos Sekondari (Tanga), nilipewa uenyekiti wa Kamati ya Taaluma, lakini baada ya miezi sita hivi nikagombana vibaya sana na mwalimu wa taaluma, ikabidi nivuliwe madaraka.
Raia Mwema: Mlitofautiana katika jambo gani na mwalimu wa taaluma?
Lissu: Ni msimamo tu. Ilitokea kwamba mwaka 1988 niko kidato cha sita, sasa kidato cha nne na cha sita kila mwaka hufanya graduation (mahafali). Wakati huo, hasa Galanos na shule nyingi za sekondari, disko hazikuwa nyingi (mara kwa mara) kama sasa.
Kipindi cha kwenda kucheza disko ilikuwa wakati wa graduation. Sasa walimu wakaamua watoto wa kidato cha nne hawatakwenda kucheza disko. Mimi niko kidato cha sita, sasa tulipanga kwenda disko Korogwe Girls. Wakaamua (walimu) kidato cha nne hawatakwenda Korogwe Girls, badala yake waletewe taarabu.
Sikukubaliana, nikaandika makala inahoji uamuzi huo. Title yake naikumbuka hadi leo, inasema; “taarab for who’s benefit?” – taarabu kwa faida ya nani?
Halafu tukafanya mpango (wanafunzi) ikabandikwa kwenye mbao za matangazo shuleni, sikuandika jina langu halisi. Walimu wakauliza, wakapeleleza nani anaweza kuandika vitu kama hivi?….wakanikamata.
Nikatuhumiwa kuleta uchochezi, nikasimamishwa shule, baadaye walinirudisha. Lakini kwa ujumla miaka ya sekondari ilikuwa mizuri, hapakuwa na njaa kama wakati huu.
Raia Mwema: Baada ya kuhitimu kidato cha sita, nini kilichofuatia?
Lissu: Nikaenda JKT Mbeya, kwanza nilipelekwa Mafinga, lakini sikukaa tukapelekwa Mbeya operesheni yangu inaitwa; Operesheni ya Programu ya Chama, mwaka 1989.
Raia Mwema: Unakumbuka nini kuhusu enzi za JKT?
Lissu: Ninachokumbuka mjadala wa vyama vingi ulikuwa umeiva na CCM hawataki vyama vingi. Ilikuwa mwaka 1989/1990, kwa Katiba ya CCM wakati huo, kulikuwa kuna mkoa unaitwa Mkoa wa Majeshi, ulikuwa mkoa sawa na mingine katika chama.
Kwa hiyo, wakatuma wajumbe wao wa Mkoa wa Majeshi kutembelea kambi zote za jeshi na JKT Tanzania nzima, kueleza msimamo wa CCM.
Waliokuja Itende JKT kwetu nawakumbuka ni Omari Mahita wakati huo ni Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, Kanali Andrew Shija na mtu mwingine simkumbuki.
Nawakumbuka Kanali Shija na Omari Mahita kwa sababu walijenga hoja kwamba haya mageuzi (vyama vingi) hayatuhusu kwa hiyo tusishabikie yasiyotuhusu; eti yanayowahusu Wazungu, Ulaya Mashariki na kwingine.
Nakumbuka nilipambana vibaya sana na Omari Mahita kwenye huo mkutano. Nilisimama kuuliza maswali nikitambua kuwa kabla hawajaja, Mwalimu Nyerere alihutubia mkutano wa Baraza Kuu la Vijana wa CCM, Mwanza na akasema wanaodhani mageuzi ya Ulaya Mashariki hayatuhusu, ni wajinga.
Kwa hiyo, nikamuuliza RPC Omari Mahita nikamwambia kwamba Mwalimu Nyerere alisema wanaofikiri mageuzi ya Ulaya Mashariki hayatuhusu ni wajinga, na wewe umekuja na timu yako unatuambia haya mambo ni ya Wazungu hayatuhusu.
Sasa mjinga ni Mwalimu Nyerere aliyesema yanatuhusu au nyie ambao mnatuambia kwamba hayatuhusu?
Raia Mwema: Bila shaka ulitumbukia katika uhasama wa ghafla na meza kuu. Hali ilikuwaje?
Lissu: Omari Mahita ni mweupe sana, basi, ghafla akabadilika rangi akawa mwekundu. Ikawa makamanda kadhaa wakasimama tayari kumshughulikia huyu serviceman…maana nilishapita ukuruta. Wakasimama kutaka kumshughulikia anayetukana maofisa wa jeshi.
Lakini kanali Shija (marehemu sasa) akasimama akanitetea. Akasema; hoja ya serviceman ni sahihi kabisa, Mwalimu ndivyo alivyosema. Kwa hiyo, hatuwezi….kusema hayatuhusu. Maana yake tayari nilianza kusakamwa pale… akasema ni kweli hatuwezi kukwepa haya mawimbi na upepo. Shija akapiga siasa, na hatimaye akaniepushia kibano.
Raia Mwema: Kwa hiyo makamanda wenyewe kwa wenyewe walitofautiana mbele yenu?
Lissu: Walitofautiana na baada ya hapo, hakuna ofisa wa JKT aliyenigusa tena. Wengi baada ya hapo wakaamini mimi ni usalama wa taifa.
Maisha yakawa mazuri. Hakuna aliyenigusa kwa sababu kama nimezungumza vile na kanali wa jeshi, kwa sababu mkuu wa kambi mwenyewe hakuwa kanali, alikuwa luteni kanali, sasa mimi nimetetewa na Kanali Shija. Kwa hiyo nilikuwa nakula shushi (mambo mteremko).
Baada ya hapo nikaenda Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Miaka ile ulikuwa huendi chuo kikuu kama si mwanachama wa CCM na sehemu ya mafunzo unayopata JKT ni pamoja na itikadi ya CCM na mnapomaliza mafunzo mnakabidhiwa pia kadi za chama. Kwa hiyo, nilikuwa mwanachama wa CCM na hiyo ni muhimu watu wakafahamu.
Lakini nilikuwa mwanachama kwa sababu tu nilitaka kusoma. Ndivyo maisha yalivyokuwa na baada ya hapo. Nilipoingia chuoni kadi haikuwa na kazi sana kwangu. Siku ya kwanza chuo kikuu hadi naondoka, mijadala yote nilikuwa mstari wa mbele kabisa pamoja na kwamba sikuwahi kuwa kiongozi.
Raia Mwema: Katika mijadala yenu chuoni hasa ile mikubwa, hoja gani unakumbuka zilitikisa uongozi au hata nchi?
Lissu: Wakati huo, dunia na nchi ilikuwa ikibadilika, hatukuwa tayari tena kutawaliwa na mfumo wa chama kimoja, eti usipokuwa na kadi ya chama huendi chuo. Nikiwa mwanafunzi, uchangiaji wa gharama za shule ulianza wakati huo.
Nilikaa mwaka mzima nyumbani kabla ya kuingia chuo kikuu kwa sababu mwaka 1989 wanafunzi wa UDSM waligoma, chuo kikafungwa.
Pamoja na kwamba sikuwa sehemu ya huo mgomo wakati huo nilikuwa JKT, lakini madhara ya mgomo yalinigusa kwa kukaa nyumbani mwaka mzima. Nilipojiunga chuo mwaka 1991, tayari vuguvugu lilikuwa kubwa sana. Na upinzani dhidi ya uchangiaji gharama za elimu ulikuwa mkubwa sana.
Raia Mwema: Mliguswa vipi na tukio la kumdhalilisha Rais Mwinyi wakati ule chuoni UDSM?
Lissu: Chuo kilifungwa kutokana na tatizo hilo mwaka 1989. Ni tukio lililotugharimu ambao ndiyo tulitaraji kwenda kuanza masomo. Tulikaa nyumbani mwaka mzima.
Raia Mwema: Katika changamoto za mageuzi chuoni, baadaye ulijiunga na chama gani baada ya mfumo wa vyama vingi kuruhusiwa?
Lissu: Kama nilivyosema, nimezaliwa rebel , na hivyo haikuwa ajabu hata kidogo mimi kujiunga na chama cha upinzani ambacho kilivutia wasomi – NCCR-Mageuzi. Ilikuwa ni hatua inayotegemewa.
Nisingeweza kuwa CCM au CHADEMA kwa sababu kilikuwa chama kisichokuwa na msimamo mkali….hawa watu ni waoga, wanaogopa kuweka msimamo mkali. Ni kama chama cha kibepari hivi na mimi kimsimamo nimekuwa Mjamaa wa mrengo wa kushoto kabisa.
Raia Mwema: Uchaguzi wa kwanza baada kuruhusiwa vyama vingi mwaka 1992 ulifanyika 1995. Ulishiriki vipi uchaguzi huo?
Lissu: Ingawa jimboni kwetu (Singida Kusini wakati huo) mwanzo hapakuwa na uchaguzi wa vyama vingi, lakini ilikuwa sehemu ya changamoto kisiasa, hata wabunge waliokuwa wakichaguliwa walidumu kwa muhula mmoja tu.
Sasa ghafla tukawa na demokrasia pana zaidi – vyama vingi, lakini kwenye uchaguzi huo (1995) ikaelekea CCM itapita bila kupingwa. Kwa hiyo nikajitokeza kugombea ubunge jimbo la Singida Kusini.
Lakini wakati naanza mchakato wa kuwa mgombea, nikapata scholarship ya Serikali ya Uingereza kwenda kusoma Master’s (Uzamili). Nikaenda shule kuripoti, nikawaambia narudi nyumbani kujaribu ubunge, nikishindwa nitarudi.
Nikatoka Uingereza kuja kugombea ubunge mwaka 1995, nikiwa na miaka 27. Nikarudi shule baada ya kushindwa. Safari yangu ya kisiasa ilianza kujitokeza kipindi hicho.
Nikamaliza shule yangu mwaka 1997, nikaoa na nikahamia Dar es Salaam (kutoka Arusha alikokuwa akifanya kazi kama mwanasheria ofisi binafsi).
Raia Mwema: Katika harakati zako, tukio gani kubwa unakumbuka lilikutia msukosuko au kuibua katika jamii?
Lissu: Tukio la kwanza kubwa ilikuwa ni mradi wa ufugaji kamba delta ya Rufiji. Mradi wa Mzungu mmoja wa Ireland anaitwa Reginald Nolan. Alipewa na Serikali ya Mkapa hekta 20,000 ili atengeneze mabwawa ya kufuga kamba kwenye delta ya Rufiji katika maeneo ambayo yana vijiji karibu vinane, watu walima na kuishi, kuna msitu ya mikoko pale. Yote ile Reginald Nolan akapewa ili atengeneze mabwawa. Sisi kama watetezi wa mazingira kupitia Chama Cha Wanasheria wa Mazingira – LEAT, tulishikia sana bango mradi wa Rufiji.
Tulifanya kazi kubwa. Niliratibu kampeni ya kimataifa kwa kila njia, ikiwamo mitandao ya kimataifa ya wanaharakati kuupinga mradi huo.
Hatimaye, Benki ya Vitega Uchumi ya Ulaya (European Investment Bank) iliyokuwa itoe mkopo kwa Nolan ambao ungedhaminiwa na Serikali ya Tanzania, wakasema hawatatoa mkopo na kwa hiyo, mradi mzima ukasambaratika.
Niliwahi kushiriki mdahalo kwenye kituo cha televisheni nchini kuhusu mradi huo wa kamba, nikiwa mimi, mmiliki wa mradi na mwandishi wa habari wa siku nyingi, James Mpinga. Kwa mara ya kwanza ndipo nilipoanza kuonekana kwenye televisheni katika kipindi cha Hamza Kasongo Hour, Oktoba 1998.
Tuliwasambaratisha kila mahali. Tukapata nyaraka za Baraza la Mawaziri zilizosema mradi ni wa hovyo, lakini umepitishwa kinyemela.
Raia Mwema: Katika mchakato mzima wa harakati hizo, uliwahi kukumbwa na vitisho vya aina fulani?
Lissu: Vitisho vingi. Unaweza kufika ofisini ukakuta bahasha yenye ujumbe wa vitisho imepenyezwa chini ya mlango.
Baada ya hapo Machi, mwaka 1999, kuna kampuni moja wenye ginnery (kinu cha kuchambua pamba). Ni kampuni ya ki-Swisi. Wakaja ofisini kwetu (LEAT) wakaomba tuwafanyie utafiti juu ya madhara wanayoweza kupata kutokana na mgodi uliokuwa ukijengwa Geita. Walitaka kubaini kama shughuli za mgodi zitaathiri shughuli zao za kusafisha pamba.
Kwa hiyo, nikapewa hiyo kazi. Nikasafiri kwenda Geita, asubuhi yake (baada ya safari) wenyeji wangu wakanipeleka wanakojenga mgodi. Nikakuta vijiji vinabomolewa kwa magreda na mbele yake wametangulia askari wenye bunduki. Kijiji kile kilipitiwa na barabara, sasa upande wa pili wa barabara yuko Mkuu wa Wilaya, Halima Mamuya, OCD na maofisa wengi.
Mkuu wa Wilaya ya Geita ameshika kipaza sauti, anawaambia wanakijiji kwamba niliwaambia mlipwe fedha (fidia) mmekataa, sasa mtajua mtakwenda wapi.
Pale kwenye shimo kubwa lenye kina cha Kilomita kama tano wanakochimba dhahabu ndipo kilipokuwapo kijiji cha Mtakuja.
Nilishuhudia mgodi wa kwanza ukianzishwa kwa kuharibu kijiji ambako kulikuwa na makazi pamoja na mazao…mahindi yanayoelekea kukomaa, na wakati huo nchi ilikuwa imekumbwa njaa kwa sababu mwaka uliopita kulikuwa na mvua za el-nino.
Hali ile ilinikumbusha wakati wa operesheni vijiji ambako nyumba yetu na za wanavijiji pamoja na mashamba viliharibiwa. Nilishangaa serikali kuharibu mashamba ya chakula. Nikaandika ripoti yangu, nikawapelekea wenye kinu cha pamba na kupendekeza kwamba tunahitaji ginnery kukaa na wananchi kijiji ili kupambana na uhalifu huo.
Nikawaambia nyie mna hela, wanakijiji watawapa ile human element, idadi ya watu ambao wanaathiriwa. Ukizungumza athari, ukaonyesha watu wanabomolewa ina value kubwa sana katika mapambano. Kwa hiyo, wanakijiji mkiwaacha wakasambaratishwa, hata nyinyi hamtabaki.
Wakaniambia sisi ni wawekezaji, nikawaambia wenzangu katika LEAT kwamba ugomvi mkubwa katika miaka inayokuja ni ugomvi wa madini.
Kwa hiyo, kutoka Geita kwenda Bulyanhulu ni mwendo wa dakika 45. Katika kuchunguza makampuni ya madini yanafanya nini kwa wananchi, kitu cha kwanza utakachokutana nacho ni Bulyanhulu. Ndio eneo ambalo kulitokea maafa makubwa zaidi.
Mwaka 1999 nikapata nafasi kwenda Marekani kuwa mtafiti katika taasisi ya World Resource Institute kwa miaka mitatu. Nikawaambia World Resorce Institute nitafanya kwa sharti moja; kwamba kazi niliyoanza kuifanya katika LEAT ya madini niendelee nayo.
Nikaondoka kwenda Marekani Septemba 1999 na kwa miaka mitatu yote mnayojajua juu ya Bulyanhulu yalipatikana katika kipindi hicho. Karibu kila mwezi nilirudi Tanzania kuendelea kutafiti suala hilo la Bulyanhulu.
Tulipata ushahidi wa picha za video na nyingine unaothibitisha kwamba watu wengi waliuawa. Hizo picha ni za jeshi la polisi na kampuni yenyewe.
Tulikuwa kila tunapopata video hizo tunazitangaza hadharani. Mwaka 2001 tulifanya press conference kubwa Maelezo kuthibitisha kwamba tunao ushahidi wa picha za video zinazothibitisha mauaji hayo kutokea.
Nilikuwa mimi na Rugemeleza Nshala. Baada ya mkutano huo, mimi nikaondoka kurudi Marekani. Lakini huko nyuma, baada ya tarehe 23, Polisi wakavamia ofisi zetu za LEAT na nyumbani kwangu wakitafuta huo ushahidi. Na wakati huo Jeshi la Polisi likasema huyu mtu ametoroka, anatafutwa na Interpol, kwa hiyo akamatwe. Wenzangu baadaye walikamatwa.
Niliporudi Marekani walinikamata na kuniweka kituo kikuu cha polisi Dar es Salaam. Nilipokuwa kituoni humo nilifanya ujanja nikaingia na simu na nikafanya mahojiano na magazeti ya Canada na Marekani usiku kucha. Kesho yake ilikuwa sikukuu ya Krismasi. Nikafuatwa na polisi, nikaambiwa napelekwa mahakamani.
Raia Mwema: Tueleze kujiunga kwako na CHADEMA, kulikuwaje?
Lissu: Kujiunga na CHADEMA mwaka 2004 sababu ilikuwa Tarime na suala la kampuni za madini. Harakati za madini Tarime nilizianza mwaka 2003.
Wakati ule mtu aliyenipokea Tarime ni marehemu Chacha Wangwe. Nilimkuta ana kesi 10 za jinai wakati huo akiwa diwani wa CHADEMA. Akaniambia; wanataka kunifunga hawa…nikamwambia hawawezi, wanakutisha tu.
Alisumbuliwa sana, na Tarime ilikuwa inatisha kama ilivyo leo. Mbowe akanipigia simu akaniomba nisaidie kisheria kumtetea Wangwe, chama kitagharimia usafiri. Kwa hiyo, nikaanza kazi ya kuwapa huduma ya kisheria na katika kipindi cha miezi minne nimetoa gerezani watu 366 waliokuwa wanatumikia vifungo.
Siku moja Mbowe akaniambia nitafute watu wengine wanataaluma ili wajiunge na CHADEMA. Nikamuuliza kwa nini unafikiria mimi ni mwanachama wa CHADEMA? Alikuwa miaka yote anafikiria mimi ni mwenzao, kumbe mimi ni NCCR-Mageuzi.
Akauliza kwa nini si mwanachama wa CHADEMA? Nikamwambia hujawahi kunipa sababu za kwa nini niwe mwanachama wa CHADEMA. Kama unataka niwe, niambie tu.
Kwa hiyo, hivyo ndivyo nilivyoingia CHADEMA. Kwa maisha yangu kwa historia yangu na msimamo wangu, mimi ni mwanahakarati, na pengine Rais Kikwete hakosei sana anaposema vyama vingine ni vya wanaharakati.
Raia Mwema: Unazungumziaje nafasi yenu Bungeni, hasa ikizingatiwa suala la idadi na ubora wenu?
Lissu: Bunge kama unaelewa sawawa linakupa nafasi ya kuibua mijadala. Siku zote sasa nimeelewa kwamba Bunge si mahali pazuri pa kutatulia migogoro, lakini ni mahali pazuri pa kuzungumzia na ku-mobilise nguvu ya umma. Hayo matatizo ya kisiasa au kikatiba, hayatatuliwi bungeni isipokuwa yanazungumzwa.
Suala la wingi, kwa maana ya idadi au ubora wa wabunge, bila kujali idadi lina umuhimu wake.
Kwa mfano; inapofika wakati wa kupitisha sheria au bajeti, hatuwezi ingawa tunao wabunge bora zaidi na wajenga hoja wazuri. Kwa hiyo, hapo ‘ujinga wa wengi’ ndipo unaposhinda. Kama unaitumia nafasi hiyo bungeni vizuri, kama ambavyo tumekuwa tunafanya, hiyo itakuwa inatusaidia kujenga nguvu kubwa nje ya bunge. Inategemea unatumiaje hiyo fursa ya Bunge.
Raia Mwema: Ulikuwa Tarime hivi karibuni. Wako wanaohoji ulikwenda kutafuta nini wakati ni eneo lenye mbunge wake.
Lissu: Labda niwajibu hao wajinga wasiojua nilikuwa nafanya nini Tarime. Kwa historia yangu na Tarime, ilikuwa ni wazi ningeenda Tarime baada ya kutokea masuala haya (mauaji) na ndugu zao kukataa kuwazika hadi uchunguzi. Ningekuwa sio mbunge pia ningekwenda Tarime. Nina historia ndefu ya mapambano ya kudai haki Tarime.
Yaliyotokea yanafamika – tulikamatwa na kuwekwa kwenye selo Tarime, tumeshtakiwa. Ni hali halisi ya Tarime. Ni eneo la vita, ni janga la kitaifa kama nilivyoeleza baada ya kuachiwa kutoka gerezani.
Tarime ya leo ni mbaya kuliko Tarime ya 2003 nilipokwenda kwa mara ya kwanza ambapo mamia ya watu wa Nyamongo walikuwa gerezani. Tarime ya leo ni ya mauaji yanayofanywa na jeshi la polisi. tangu tuwashinde (CCM) uchaguzi. Mauaji ya kwanza Tarime yalifanyika Julai 20, 2005. Hadi kuua hawa wa juzi watano, sasa wamefikia watu 28 waliouawa kwa kupigwa risasi mchana kweupe.
Raia Mwema: Lakini kiini cha tatizo nini? Je, ni mwekezaji au jeshi la polisi?
Lissu: Tatizo ni mwekezaji, polisi na Serikali ya Tanzania. Kusingekuwapo mwekezaji, watu wasingeuawa.
Raia Mwema: Lakini kama tatizo ni pamoja na polisi au serikali kuna migodi mingine mauaji hayaendelei kama Tarime?
Lissu: Katika sekta ya madini unakuja na umwagaji damu. Bulyanhulu, Tarime, Geita, Nzega hakuna mahali ambapo wawekezaji wameweka mgodi wa dhahabu wa kisasa bila kuangamiza uchumi wa wenyeji, bila kuwaondoa kwa mabavu ya kijeshi.
Raia Mwema: Kifanyike nini?
Lissu: Ni mambo mawili ya kuchagua. Kwanza, je, tunataka huyo anayeitwa mwekezaji achume mali na inunuliwe kwa damu za Watanzania? Inunuliwe kwa Watanzania kukosa haki na kwa uchumi wa Watanzania kusambaratishwa? Au tuamue kwamba maisha ya Watanzania ni bora zaidi kuliko dhahabu.
Kwa maoni yangu, haiwezi bei ya dhahabu ikawa sawa na maisha ya mtu mmoja. Watanzania wameshauwa kwa risasi na kwa kunywa maji ya sumu yanayotokana na mwekezaji. Tarime imejaa vijana wanaoshitakiwa kwa kesi za ugomvi na mgodi, lakini sasa hivi wanashtakiwa kwa kesi za mauaji au uhalifu wa kutumia silaha!
Wakati nakwenda Tarime kwa mara ya kwanza, kesi zilizokuwa zikifunga watu zilikuwa uchochezi na kuvamia eneo la mgodi, lakini leo kesi za Tarime ni mauaji. Hata ukikamatwa kwa kurushwa jiwe ambalo halijampiga mtu yeyote, utashtakiwa kwa mauaji au uhalifu wa kutumia silaha!
Na unashtakiwa kwa hayo makosa mawili kwa sababu huwezi kupewa dhamana. Kwa hiyo, polisi wasipofanya upelelezi utafia gerezani.
Nilikamatwa Tarime nikakaa gerezani. Naweza kuthibitisha kuwa Tarime kuna watu zaidi ya 400 wanaokabiliwa na kesi za mauaji.
Sasa njoo huku ambako hakuna mgodi, leo biashara ya teksi Tarime mjini ni biashara ya mapolisi kwa sababu wafanyabiashara wa kawaida pale mjiini aidha wako gerezani wakikabiliwa kwa mauji au wengine wameuawa.
Selo niliyofungwa mimi Tarime inatumika kwa kitu kimoja tu, nimeambiwa kuna watu wengi sana wameuawa, wameumizwa sana. Kuna mtu mmoja amepigwa risasi tano miguuni kwenye kituo cha polisi na mkononi amepigwa risasi mbili, na mkono umekatwa.
Kuna watoto. Kuna mtoto wa miaka 12 selo niliyolala mimi. Bunge hili limepitisha sheria mwaka juzi, sheria ya mtoto inayosema mtoto wa miaka 18 hawezi kupata adhabu ya kifungo.
Huyu mtoto ana miaka 12 anakaa kwenye gereza na wafungwa watu wazima waliopatikana na hatia. Napeleka hoja binafsi bungeni kuomba iundwe kamati teule ya Bunge kuchunguza suala hili.
TANBIHI: Makala ya gazeti la Raia Mwema la mwaka 2012
Filed under: Siasa Tagged: CHADEMA, Lissu, Tanzania

Je, kifo cha Jumbe chaweza kututanabahisha Wazanzibari?

Nilianza kumjuwa Mzee Jumbe wakati nikiwa mdogo sana miaka ile ya ’70 na mwanzoni mwa ’80. Kwanza ilikuwa kupitia magazeti na picha za kalenda mbalimbali zilomuonesha akishiriki shughuli za kimaendeleo visiwani Zanzibar. Hatimaye, mwanzoni mwa miaka ya ’80, Mzee Jumbe alitembelea kijijini kwetu kukagua shughuli za kilimo kwenye bonde maarufu kisiwani Pemba, bonde la Makwararani. Pamoja na udogo niliokuwa nao kipindi hicho, bado nakumbuka tukio la Mzee Jumbe kumtunza pesa mpiga msewe mashuhuri katika wilaya ya Micheweni, Mzee Bin Malengo, ambaye alikuwa gwiji wa ngoma hii. Tendo hili lilikuwa la heshima kubwa kwa gwiji huyo kiasi cha kuwa gumzo kwenye wilaya nzima ya Micheweni, na likawa kichocheo cha ngoma hii kuenziwa na kuendelezwa hadi leo hii, tofauti na ngoma nyingine nyingi za kiutamaduni zilizokufa.
Filed under: Siasa Tagged: Jumbe, maalim seif, shein, Zanzibar

La mkono wa Maalim Seif na uhalisia wa hisia
Hisia ni kitu ambacho kila kiumbehai anacho kutegemea na hukionesha kulingana na mazingira husika. Tafsiri ya hisia hizo ni za aina mbili – chanya na hasi – kama vile ambavyo kinachozipelekea hisia kililivyo. Hisia chanya ni zile ambazo mtu akiwa nazo huonekana hali ya bashasha, furaha, tabasamu na hata kicheko; na hisia hasi hujidhihirisha kwa hali ya hasira, chuki, mikunjo ya uso na hata kilio.
Hisia ni sehemu ya maumbile yetu na mtu anapokuwa nazo – ziwe hasi ama chanya – huwa hajakiuka ubinaadamu wake, isipokuwa kila mtu anavyozidhibiti hisia zake chanya huonekana na wengine kwamba amejiweza zaidi. Hapa nazungumzia kitendo cha Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, kukataa kuinua mkono wake kuupokea mkono wa Makamu wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar (CCM), Dk. Ali Mohamed Shein, siku ya maziko ya aliyekuwa rais wa pili wa Zanzibar, Mzee Aboud Jumbe Mwinyi.

Ninachosema ni kuwa hisia za Maalim Seif ni maamuzi ya nafsi yake juu ya kuficha hisia zake na kiwango cha kuzificha na kuzifichua ni hukumu yetu sisi tulioziona. Lakini ikiwa tunafahamu kuwa Maalim Seif anaamini kwamba Dk. Shein ni hasimu wake kwa kuwa amemdhulumu haki yake, basi hatuna budi pia kukufahamu kule kuonyesha kwake hisia zake.
Tusiwe wasahaulifu kwa matukio ya watu mashuhuri kama yeye au zaidi yake, Maalim Seif. Kiongozi huyu mwenye ufuasi mkubwa visiwani Zanzibar si mtu wa kwanza kuonyesha hisia zake za hasira kwa mtu anayemchukulia kuwa na sifa (au tuseme ila) alizonazo. Kinyume chake, naweza kusema, Maalim Seif ni wa mwisho hadi kufikia siku ya maziko ya Marehemu Mzee Jumbe kwa watu mashuhuri kukataa kutoa mikono kwa mahasimu wao.
Kwa kuwa tuko katika masiku saba ya maombolezo ya kifo cha Mzee wetu Jumbe Mwinyi, basi nitakuonyesha matukio saba ya watu walionyesha hisia zao kwa kukataa kuwapa mikono mahasimu wao au wasiowapenda, miongoni mwao wakiwemo marais wa nchi kubwa duniani hadi wanariadha na wachezaji mpira mashuhuri.
George W. Bush mwaka 2008
Mnamo tarehe 22 Novemba 2008, mitandao mbalimbali duniani iliripoti tukio la mkutano wa wakuu wa nchi za mataifa 20 yenye nguvu za kiuchumi, G20, ambapo Rais George W. Bush wa Marekani aliwawapita wakuu wenzake wa nchi bila kuwapa mikono na hata hao wakuu wenzake wa nchi hawakunyoosha mikono kumpa Bush.
Wine Bridge mwaka 2010
Mnamo tarehe 28 Machi 2010, iliripotiwa katka gazeti la Daily Mail la Uingereza kwamba mchezaji wa Manchester United alikataa kumpa mkono rafiki yake na mchezaji mwenzake waliocheza pamoja katika timu ya Chelsea ya Uingereza, John Terry. Sababu ya kuonyesha hisia zake hizo na kushindwa kumpa mkono Terry zinaelezwa ni kwamba ni pale ilipogundulika kwamba John Terry alikuwa anatoka kimapenzi na mpenzi wa zamani wa Wine Bridge.
Luis Suarez mwaka 2012
Mnamo tarehe 12 Februari 2016 wakati timu mbili hasimu yaani Manchester United na Liverpool zilipokutana kwa ajili ya mchezo wa ligi kuu ya uingereza Luis Suarez alikataa kumpa mkono Patrice Evra wa Manchester United kwa kuwa alikuwa hampendi kutokana na weusi wake, hivyo alishindwa kuzuiya hisia zake na kukataa kumpa mkono.
Antony Ferdinand mwaka 2012
Mnamo tarehe 16 Septemba 2012 mchezaji mpira wa QPR alikataa kupeana mkono na nahodha wa timu ya Chelsea John Terry wakati timu hizo zilipokutana kwa ajili ya mchezo wao ligi kuu ya uingereza, ambapo sababu iliyoelezwa ni kwamba John Terry alifanyia ubaguzi wa rangi Antony Ferdinand ndipo na yeye akaonyesha hisia zake za kuchukizwa.
Robert Mugabe mwaka 2015
Tarehe 28 Aprili 2015 rais Robert Mugabe wa Zimbabwe alikataa kupokea mkono na kiongozi/mfalme wa Wazulu wa Afrika ya Kusini, kwa kitendo cha mfalme huyo kuhamasisha ubaguzi na mauaji dhidi ya wageni wanaoishi Afrika ya Kusini.
Rais Francoise Hollande wa Ufaransa na polisi mwaka 2016
Tarehe 17/06/2016 imeripotiwa kwamba, ofisa wa polisi wa ngazi ya juu wa Ufaransa alikataa kumpa mkono Rais Francoise Hollande wakati wa ghafla ya kuwapa pole maaskari hao baada ya wenzao wawili kuuawa na shambulio la Dola la Kiislam (ISIS). Na baadae polisi huyo alipohojiwa na kituo cha utangazaji cha BBC alisema hakutaka kumpa mkono kwa sababu kuna matatizo mengi wanayokabiliana nayo ndani ya jeshi la polisi.
Islam El Shehaby wa Misri
Katika michezo ya Olimpiki ya Rio 2016, imeripotiwa kwamba mcheza Judo wa Misri alikataa kumpa mkono mchezaji mwenzake wa Israel kwa kuonyesha hisia zake kitaifa juu ya ugomvi uliopo baina ya Waarabu na Waisrael katika Mashariki ya Kati.
Matukio kama haya ya kuonyesha hisia yapo mengi sana katika jamii kama kweli tutaamua kuyafatilia. Sasa na hili la Maalim Seif kutokumpa mkono Dk. Shein si kioja. Ni jumla ya kuonesha kile anachokiamini kwamba hakiko sawa.
Filed under: Siasa Tagged: Dk. Shein, maalim seif

Doyo tumekusikia, tunakuhifadhia

Ndio maana pia, ingawa wengi miongoni mwetu tunaamini katika dini tulizozichaguwa kuwa waumini wake, lakini hayupo kati yetu aliyepata kumshuhudia Mtume Issa (Yesu) au Nabii Muhammad akifikisha Neno la Mungu, bali ujuzi na uelewa wetu juu ya imani zetu za kidini umetokana na mapokeo yaliyotokana na vitabu vyenye kubeba ujumbe huo wa kiimani.
TANBIHI: Mwandishi wa makala hii ni mwandishi wa habari wa kujitegemea.
Filed under: Siasa

Lipumba na la kuvunda
Hufika muda tunalazimika kukubali matokeo. Inawezekana kuikubali hali hiyo kwa shingo upande au maumivu makali yasiyomithilika. Hata hivyo, maumivu na sononeko hilo haliondowi uhalisia wa mambo. Kwamba la kuvunda halina ubani hata hikima na juhudi kubwa zikitumika.
Chanzo cha maumivu na sononeko la wengi huwa ni mapenzi ambayo hupelekea mjengeko wa matumaini yenye kuegemezwa kwa kitu au mtu fulani. Kukosekana kwa kile kilichotarajiwa hupelekea kuibuka mengi, yakiwemo kukata tamaa au hata fikra za kujitowa uhai. Na hata baada ya hayo, hakika jitihada haishindi kudura!
Na mimi pia na nina maumivu – nataka nikiri tangu mwanzo – na maumivu yangu yanarudisha fikra zangu miaka kadhaa nyuma. Namkumbuka mmoja wa waasisi wa Chama cha Wananchi (CUF), Marehemu Mzee Shaaban Khamis Mloo. Namkumbuka mzee huyu siku alipopanda juu ya jukwaa na kumkabidhi chama hiki Profesa Ibrahim Haruna Lipumba pale kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam, ambapo alimuusia kwa kumwambia: “Ibrahim, nakukabidhi chama, kisimamiye. Ibrahim nakukabidhi wananchi wanyonge walioumizwa na utawala dhalimu, wapiganiye. Ibrahim nakukabidhi umma huu ulio mbele yako, shirikiana nao ili kuiletea nchi hii ukombozi wa kweli baada ya ule wa bendera, ambao umeshindwa kukidhi matarajio yao. Utaweza kulifanya hilo, kama ukiweza kushirikiana na wenzako ndani ya chama chetu cha CUF, ambao wana dhamira ya dhati ya kupigania haki na ustawi wa Watanzania hawa. Mungu akuafikishe.” Huu ndio usia niukumbukao toka kwa Marehemu Mzee Mloo kwenda kwa Lipumba siku akimkabidhi uenyekiti wa CUF.

Mapenzi yangu kwa Profesa Lipumba na CUF ni makubwa na yenye ukumbi mpana moyoni mwangu. Naamini, si peke yangu. Tupo kwa malaki kama si mamilioni, walio hai na washaotangulia mbele ya haki. Wengi tumeathiriwa na chama hiki kwa namna moja au nyingine. Wapo waliopoteza maisha, waliopata ulemavu wa kudumu na wapo wengine ambao ndio wengi waliojikuta magerezani kwa mapenzi yao kwa Lipumba na kwa CUF.
Hapa nawakumbuka makumi ya watu waliokatishiwa uhai wao kutokana na mapenzi yao kwa chama hiki kwenye maandamano ya Januari 26 na 27 na yeye Profesa Lipumba na wenzake walioumizwa vibaya. Namkumbuka mzee wangu mmoja ambaye ni mkaazi wa Mbagala ambaye amepata ulemavu wa kudumu na kijana mdogo ambaye alipigwa risasi pale maeneo ya Temeke kwenye harakati za kukisimamisha chama hikii kwenye maeneo mbalimbali. Bado kichwani mwangu zimejaa kumbukumbu za namna vijana walivyojitolea kusafiri kwa malori na mabasi toka Dar es Salaam hadi Tanga, Dodoma mpaka Mwanza kukiimarisha chama hiki kwa gharama zao wenyewe. Bado nakumbuka ibuko la matawi kama vile Chechenya, Bosnia, Ukanda wa Gaza, Hamas na mengine mengi ambayo yaliibuwa hamasa kubwa miongoni mwa vijana. Jee, viongozi wakuu wa CUF, mumeshasahau haya?
Matumaini ya sisi wengine yakaaza kupotea juu ya mustakbali mwema wa CUF miaka kadhaa iliopita. Hii ilitokana na mienendo ya baadhi ya viongozi wa chama hichi, ambao walionekana wazi kupigania maslahi binafsi na si yale mapana na yenye manufaa kwa kila mdau wa chama hichi. Wapo miongoni mwao waliowaza na kujaa zaidi tamaa ya vyeo ili kufanikisha ya kwao, huku wakisahau lengo na madhumuni ya kuanzishwa CUF. Lakini wapo pia ambao waliumizwa sana na chama hiki kiasi cha kuamuwa kuachia nafasi zao za kiuongozi kwa lengo la kulinda heshma zao. Hawa walikhiyari wakauze chips mitaani kuliko kusaliti dhamira na malengo ya chama hichi. Jiulize, kwa mfano, nini kilimuondoa Said Miraj Abdullah, kijana shupavu na makini, mtu aliyejitolea hadi kupata ulemavu wa kudumu sababu ya CUF?
Wakati Profesa Lipumba akitangaza kujivuwa wadhifa wa uenyekiti wa chama chake mwezi Agostu 2015, wengi waliumia, kwa vile walikuwa wamejenga imani kwamba ni jambo gumu kuweza kutokea mwingine wa kuvaa viatu vyake au wa kujaa ndani ya kiti chake cha uenyekiti ambacho alikaa na kujaa ndani yake. Waliumizwa pia na wakati wenyewe alioamua kufanya hivyo, kwani ni wakati ambao kwa hakika CUF ilikuwa ikihitaji uongozi wake.
Hata hivyo, waliumia zaidi pale alipotangaza kurudi tena kwenye nafasi ile ile ambayo alishaamuwa kuiwacha. Na hapa waliumizwa kutokana na namna alivyoamuwa kuirejeshea hiyo. Kwamba kwa namna alivyoamuwa kuirudia, kurudi kwake kulibeba masuali mengi vichwani mwa wenye kutafakari.
Kuteleza, kwa hakika, si udhaifu kwa mwanaadamu. Ndilo pambo lake. Wengi waliamini kuwa Profesa Lipumba alikuwa ameteleza kama binaadamu, pale alipoamua kukitelekeza chama chake katika wakati kama ule muhimu kwenye siasa za nchi. Lakini inaonekana alipoamua kurudi kwenye nafasi yake ya uwenyekiti, jambo la kwanza ambalo amelitaka lifunikwe ni kutuaminisha kwamba hakuwa ametenda kosa lolote kuachia wadhifa wake katika hali ile na kisha kukaa nje ya chama kwa zaidi ya miezi kumi, akiwa hakushiriki kazi yoyote ya kichama ndani ya kipindi hicho chote. Anataka tuamini kuwa alikuwa sahihi kukiacha chama muda aliotaka kukiwacha, alikuwa sahihi kutokujishughulisha na chama hiki muda wote ambao hakujishughulisha, na sasa yuko sahihi kurudi kwenye nafasi ya uwenyekiti na kufanya apendavyo!
Kama si hivyo anavyotaka tuamini, basi Profesa Lipumba alikuwa na njia rahisi ya kurudi kutuongoza na ambayo ingelijenga imani kwa wenzake wa karibu ambao amekuwa nao tangu hajawa mwenyekiti mpaka amekuwa, nayo ni ile ya kufata taratibu ambazo zimewekwa kikatiba. Kinyume chake, si jambo jepesi kuamini kwamba pale ambapo mume anadai kumrejea mkewe katika hali ambapo kile kilichomfanya kumpa talaka kwa mara ya kwanza, bado kingalipo.
Kama mtu ambaye ana nafasi kubwa mioyoni mwa wengi na mwenye dhamira ya kututetea kama alivyousiwa siku ile pale Mnazi Mmoja na Mzee Mloo, hivi Profesa Lipumba alishindwa nini kujaza fomu kuomba tena uenyekiti penye dhamira njema juu ya anaowapigania? Kwa nini aliamua kuuwacha njia panda ule umma aliokabidhiwa na Mzee Mloo? Kweli ametawaliwa na ghadhabu kiasi cha kusahau uzito na umuhimu wa kauli ya Mzee wetu huyu?
Kwa hakika, uamuzi wa Profesa Lipumba umewakatisha tamaa wengi ambao walimuimbia na kushangilia kila walipomuona. Umewaumiza wengi ambao walikubali kupigwa na jua, mvua na hata mabomu na risasi za moto kwa ajili yake na CUF yao. Imewauma na kutafishi nafsi zao kwamba hata viongozi wakubwa wenye kuheshimika kiimani kama vile masheikh na mapadri hakutaka kusikia nasaha zao na badala yake akaendeleza msimamo ambao leo umeacha sononeko kubwa miongoni mwao.
Kitu kimoja kipo wazi: nacho ni kuwa yaliyomfanya akiwache chama na kumsuta dhamira, bado yapo. Ushirikiano wa CUF na vyama vingine chini ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) bado upo. Edward Lowassa wa CHADEMA, ambaye eti Profesa Lipumba anataka iaminike kuwa ndiye kisa cha yeye kuiwacha CUF mkondoni, bado yupo na bado ana dhamira ya kugombea tena urais mwaka 2020, na huenda UKAWA ikamuunga tena mkono. Lakini Lowassa huyu alimleta yeye mwenyewe kwenye UKAWA, na si mwengine.
Binafsi siamini kwamba kama kweli Profesa Lipumaba ana dhamira ya kuiondowa CCM madarakani, kwani uzoefu wa miaka 25 ya chaguzi za vyama vingi umetuonesha kuwa sisi wapinzani hatuwezi kuiondoa CCM kama hatukusimama pamoja. Inavyoonekana ni kuwa Profesa Lipumba anataka CCM iendelee kubakia madarakani, naye anapendezewa kuitwa mpinzani wa kudumu.
Pamoja na hayo, lazima tukiri kwamba ongezeko kubwa la wabunge wa upinzani kwenye bunge letu limetokana na juhudi za akina Profesa Lipumba na wenzake, ambayo waliwekeza kwa muda mrefu kwenye mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara. Ni kutokana na kazi hiyo, ndiyo maana ikawa rahisi kwa upinzani kuachiana maeneo na kisha kuungana mkono kwenye baadhi ya majimbi, jambo lililopelekea mafanikiyo haya ya sasa. Lakini leo kuwa na mwenyekiti wa chama ambaye jukumu lake kuu alilojipa ni kukiondoa chama hiki kwenye umoja uliouasisi mwenyewe na ambao umeleta faida maradufu kwa chama chake hicho, kunataka upumbavu wa kiwango cha juu kumkubali, acha mbali kumuamini?
Ni muda mrefu Watanzania wamekuwa wakisisitiza na kulilia vyama kuungana ili kuleta tija na changamoto kwenye bunge letu, jambo ambalo hatimaye limewezekana. Huu ulikuwa mwanzo mzuri wa kuanza safari ya kukiondowa chama tawala madarakani. Ila safari hii ingefanikiwa iwapo viongozi wangetanguliza mbele harakati na mipango ya kufanikisha hilo, huku wakisahau suala la nani awe raisi na ile falsafa ya kwamba kwenye siasa hakuna rafiki wala adui wakudumu. Viongozi hawakupaswa kugawana fito na badala yake wangeshikamana na kuimarisha jengo ambalo lingewasitiri wote.
Jitihada haishindi kudura, nimetangulia kusema. Mengi yalifanyika ili hali hii ya sasa isijitokeze, lakini ikashindikana, na sasa CUF inaonekana kugawika vipande vipande. Kwa njia nyepesi, CCM imesaidiwa kumaliza kazi ambayo iliipigania kwa miongo mitatu.
Huu ni usaliti na ubaya usiomithilika. Kila aliyehusika na anayeendelea kuhusika, akumbuke kwamba bendera ya mwanzo kupandishwa mlingotini baada ya kuasisiwa kwa chama hiki kule kwenye kijiji cha Shumba ya Mjini kisiwani Pemba, ilimwaga damu na kuondoka na roho ya mpandishaji wa bendera hiyo. Alipigwa risasi na kufariki papo hapo.
Wallah thumma Wallah, Mungu hatomuacha msaliti yeyote. Wakati wakipapurana na kukifikisha chama ambacho wengi wamekijengea matumaini hapa kilipo, kuna watoto ni mayatima na mama zao ni vizuka. Bado pana kumbukumbu ya vijana wabichi waliotolewa roho kwenye maandamano ya Januari 26 na 27.
Labda hawa wanaokisongoa roho chama hiki wamewasahau wahanga hao na ndio chimbuko la kukigawa chama mapande kwa maslahi binafsi. Juhudi kubwa zilifanywa kuwarudisha kwenye msitari lakini wakashindwa kutanabahi. Na sasa hakuna jinsi ila kutafunwa na ubaya wa dhambi hii.
Filed under: Siasa Tagged: cuf, Lipumba, Tanzania, Zanzibar

Sababu tatu za CUF kupigwa vita na dola
Nimeichukuwa tena na kuisoma kwa makini zaidi taarifa ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF) ya tarehe 15 Septemba 2016 iliyotolewa mbele ya waandishi wa habari katika ukumbi wa habari wa Bunge hilo mjini Dodoma na ambayo ilizungumzia kadhia nzima ya mgogoro wa mwenyekiti mstaafu wa chama hicho, Profesa Ibrahim Haruna Lipumba. Sehemu ya taarifa hiyo ilisomeka hivi: “Tumepata taarifa kutoka kwa vyanzo vinavyoaminika serikalini kuwa kuna njama zinazopangwa na washindani wetu wa kisiasa Chama Cha Mapinduzi (CCM), vyombo vya ulinzi na usalama na serikali ya CCM kutaka kuitumia ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa kumtangaza Prof. Ibrahimu Lipumba kuwa Mwenyekiti halali wa CUF. Dhumuni la yote hayo ni kutaka kukiyumbisha chama chetu na kutupandikizia mgogoro usiopaswa kuwepo. Kama kitendo hicho kikifanyika kitakuwa kinyume kabisa na katiba, kanuni na taratibu za chama chetu, lakini kitakuwa kinyume na sheria ya Vyama vya siasa namba 5 ya mwaka 1992 ambayo haitoi mamlaka yoyote kwa Msajili wa vyama vya siasa kukipangia chama cha siasa viongozi wake.”
Kwa ufupi, taarifa nzima ya siku hiyo ya wabunge hao ilikuwa ni kueleza wasiwasi wao huo kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, kuitumia ofisi yake kinyume cha sheria na taratibu ili kukidhi matakwa ya kukiharibu chama chao. Lakini kama lengo lao lilikuwa ni kuzuwia hilo walilohofia lisitokee, basi hawakuweza, kwani siku tisa tu baadaye, Jaji Mutungi aliwasilisha barua yake kwa CUF, barua ambayo inamtambua Lipumba kuwa mwenyekiti halali wa CUF, licha ya msajili huyo kutambuwa pia kwamba Lipumba aliwahi kukiandikia chama chake barua rasmi ya kujiuzulu uongozi wa chama hicho.

Kitendo hiki cha Jaji Mutungi kinaweza kumshawishi yeyote kwamba tuhuma za wabunge wa CUF walizozitoa tareh 15 Septemba 2016 dhidi yake sasa zinaanza kupata mashiko. Tuhuma hizi zikaongezewa nguvu pale jeshi la Polisi lilipoyasindikiza maandamano ya Lipumba kuingia Ofisi Kuu za CUF Buguruni kwa nguvu kwa kuvunja mageti na milango ya ofisi hizo na kufanya uharibifu wa mali na kuwajeruhi walinzi huku polisi wakibaki kimya bila kutoa kemeo lolote.
Kwa hivyo, ni wazi kuwa CUF kama chama inapambana kwa sasa na maadui wakubwa kuliko Lipumba na kundi lake tu. Mikono inayomshikilia Lipumba kwenye hili ina mafungamano ya moja kwa moja ya vyombo vya dola, ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, na hapana shaka makundi mengine yenye maslahi na kile anachokifanya yeye, Lipumba. Hilo liko wazi. Lisilokuwa wazi ni sababu ambazo zinaifanya CUF ipigwe vita hivi vikubwa wakati huu na wapigaji wenyewe wawe hawa tuliowataja.
Makala hii imeziona sababu tatu kuu, kati ya nyingi nyenginezo zinazoweza kuwepo, zote zikihusiana na mafanikio ya CUF: kwanza ni mafanikio yake ya kuthibitisha kuwa ni chama pekee cha siasa ambacho hasa cha kitaifa, pili ni mafanikio ya CUF kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2o15 ule wa Marudio wa Machi 2016 na, tatu, ni mafanikio yake katika jukwaa la kimataifa baada ya chaguzi hizo mbili.
CUF kuwa chama halisi cha kitaifa
Unaweza kujiuliza kwa nini iandamwe CUF na sio CHADEMA, ambacho ni chama chenye wabunge wengi zaidi na ndicho kilichojizolea ushindi mkubwa kwenye uchaguzi wa 2015 upande wa Tanzania Bara kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA)? Ni CHADEMA iliyopata wabunge 70 kiujumla katika uchaguzi huo, huku CUF ikiwa na wabunge 48 tu kwa Bara na Zanzibar.

Ukweli ni kuwa, licha ya Tanzania kuwa na jumla ya vyama 22 vyenye usajili wa kudumu, vingi vyao vinaitwa vya kitaifa kwa jina tu, vikionesha utaifa wake kwa kushiriki chaguzi zinazoandaliwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) na ile ya Tanzania (NEC) na au kutoa matamko yanayohusu nchi, ni vyama viwili tu pekee ndivyo vilivyoweza kuthibitisha kwamba kweli ni vya kitaifa.
Kwa muktadha wa makala hii, utaifa wa chama ni kuwa kwake na wafuasi na wanachama wa kutosha pande zote mbili za Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ambao wanakipa chama hicho uwezo wa kushinda angalau kiti kimoja cha ubunge wakati uchaguzi mkuu pindi unapoitishwa.
Tangu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania irudi katika mfumo wa demokrasia ya vyama vingi mwaka 1992, katika chaguzi zote zilizofanyika kuanzia ule wa mwaka 1995, 2000, 2005, 2010 na uliomalizika mwaka jana 2015, ni chama tawala (CCM) na CUF pekee ndivyo vinavyothubutu kushinda viti vya ubunge pande zote mbili za Jamhuri hii.
Hivyo katika upinzani wa Tanzania, CCM inaiangalia CUF kuwa ndiye adui wake wa karibu na hatarishi zaidi kuliko chama chengine chochote kile. Hata pale UKAWA ilipojaribu kutaka kutengeneza adui wa pili, kwa mfano, pale walipokubaliana kuachia jimbo la Kikwajuni, kisiwani Unguja, waachiwe CHADEMA ili chama hicho nacho kiweze kupenya kidogo kidogo upande wa Zanzibar, lakini hilo halikuwa. CCM ilihakikisha kuwa CHADEMA haiingii Zanzibar, na hivyo kuendelea kukifanya kuwa chama kikuu cha upinzani Tanzania Bara tu, licha ya CUF kuifungulia milango.
Lakini UKAWA iliyoshindwa kufungua milango kwa vyama vyengine kuingia Zanzibar, bado iliimarisha zaidi CUF kwenye nafasi yake ya kuwa chama cha kitaifa kuliko chama chengine chochote kwenye umoja huo kwa upande wa Bara pia. Kabla ya uchaguzi huo wa Oktoba 25, CUF ilikuwa imeshapoteza nguvu zake upande wa Bara, ikiwa na wabunge wawili tu – wa Kilwa na Lindi Mjini. Lakini kupitia UKAWA, CUF ikapata viti 10 upande wa Bara.
Mafanikio haya, hapana shaka yoyote, yameitisha sana CCM na, kwa mara nyengine, imejithibitishia kuwa adui yake mkubwa kitaifa ni CUF tu. Ndiyo maana si jambo la ajabu kuwa inatumia nguvu zake zote, ikisaidiwa na mawakala wake ndani na nje ya dola, kuhakikisha kuwa inaiangamiza CUF kabla ya 2020.
Mafanikio ya Oktoba 2015 na wa Marudio Machi 2016
Kila mfuatiliaji wa uchaguzi wa Zanzibar wa mwaka 2015 anakubali kuwa huo ulikuwa ni wa kwanza kuwa na unafuu kushinda chaguzi zote zilizofanyika Zanzibar tangu kurudishwa kwa siasa za vyama vingi mwaka 1992. Waangalizi wote wa kitaifa na kimataifa waliusifu uchaguzi huu wa tarehe 25 Oktoba 2015 kuwa ulikuwa uchaguzi huru, wa haki na uwazi.

Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyokuwepo kabla ya uchaguzi huo ilijitahidi pakubwa kuandaa mazingira ya uchaguzi unaokidhi viwango vya kilimwengu, licha ya matatizo ya hapa na pale.
Lakini siku tatu baada ya kura kupigwa, yaani Oktoba 28, Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salum Jecha, aliufuta uchaguzi wote, baada ya kusuasua katika zoezi la utoaji matokeo licha ya yeye mwenyewe kuusifu uchaguzi huo mbele ya waangalizi wa kimataifa.
Mpaka anaufuta uchaguzi huo, tayari nusu na robo ya majimbo ya uchaguzi yalishahakikiwa na kuwekwa sahihi na pande zote za vyama vilivyoshiriki uchaguzi, ambapo majimbo 40 yalihakikiwa na kukubalika, majimbo 31 yalishatangazwa matokeo yake, na majimbo yaliyobakia yalikuwa ni 13 pekee kutimiza majimbo 54.
Baada ya kufutwa kwa uchaguzi huo, chama cha CUF, ambacho kinaaminika na wengi kuwa mgombea wake wa urais, Maalim Seif Sharif Hamad, alikuwa amepata ushindi wa 53%, kkilizikataa hatua za maamuzi yote mawili, kuanzia lile la kufutwa kwa uchaguzi na pia hatua ya kurejewa kwa uchaguzi mwengine wa Machi 20. ‘Uchaguzi wa Machi 20’ ndio uliomuweka madarakani Dkt. Ali Mohammed Shein.
Maamuzi hayo yalikataliwa na taasisi mbalimbali za waangalizi wa uchaguzi wa kitaifa na kimataifa, miongoni mwao ni Jumuiya ya Madola (Common wealth), Jumuiya ya Ulaya (European Union), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC), ambayo kwa sasa mwenyekiti wake ni Rais John Pombe Magufuli wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mafanikio haya ya CUF ya waziwazi kwenye uchaguzi ambao unatazamwa kama wa haki na huru zaidi kuwahi kufanyika Zanzibar, hapana shaka ni donda ndugu kwenye kiwiliwili cha CCM. Tangu kumalizika kwa uchaguzi wa Oktoba, CCM imejikuta haina uso wowote mbele ya yeyote, wa ndani na wa nje, kila mtu mwenye kujiheshimu, amekuwa upande wa CUF. CCM imekuwa peke yake. Ndiyo maana itafanya iwezalo kuhakikisha kuwa CUF, mshindi halali wa uchaguzi huo, anaporomoka iwe iwavyo!
Mafanikio kwenye jukwaa la kimataifa
Mara baada ya kushindikana kwa mazungumzo kati ya Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, na viongozi wakuu wa sasa na wa zamani wa Zanzibar kuhusiana na uchaguzi huo na uamuzi wa kibabe wa CCM kwenda kwenye uchaguzi wa Machi 20, CUF iliamua kuachana kabisa na kuwashika miguu CCM na badala yake ikageukia jumuiya ya kimataifa.

Hilo lilifanyika kimahisabu na hatua kwa hatua, kwanza kwa kuwafuata mabalozi wa mataifa ya kigeni na asasi za kimataifa ndani ya Tanzania, kisha ikawa kuyafuata mataifa makubwa duniani huko huko yaliko. Kila hatua moja iliyopiga, CUF ilikuwa inajijengea heshima na jina mbele ya uso wa dunia, hasa kwa kuthubutu kwake kuwatuliza wananchi waliokuwa na hasira na badala ya kuwajaza barabarani kuandamana, wakawafanya wabakie majumbani mwao kungojea suluhu ya amani.
Maalim Seif na ujumbe wake wakaranda kote – tangu Marekani kwenye Umoja wa Mataifa hadi Uingereza kwenye Jumuiya ya Madola hadi Ubelgiji kwenye Umoja wa Ulaya hadi Uholanzi kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC). Na mote humo walipokelewa na kufanya mazungumzo ya kina na wahusika. Wakasikilizwa, wakafahamika.
Miongoni mwa matokeo ya karibuni zaidi ya ziara hizo kwenye jumuiya ya kimataifa yakawa ni tamko rasmi la kimaandishi lililowasilishwa kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon mnamo Septemba 2016 Muungano wa Vyama vya Kiliberali Duniani (LI) juu ya uvunjwaji wa haki za binaadamu na misingi ya kidemokrasia visiwani Zanzibar.
Tamko hilo lilikabidhiwa kisheria kwa kutumia ajenda Namba 3 ya Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja la Umoja wa Mataifa, likielezea kwa dhahiri na shihiri kila ambacho kilitokea Zanzibar kuanzia Uchaguzi wa Oktoba 25, 2015 na ule wa marudio wa Machi 20 mwaka huu pamoja na mikanda ya video na picha za matukio yote ambayo Umoja huo wa Kiliberali ulijiridhisha kwamba ni kweli haki za binaadamu zilikiukwa Zanzibar.
Sasa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayotawaliwa na CCM imekalia kuti kavu mbele ya jumuiya ya kimataifa na aliyeifanya iwe kwenye hali hiyo ni CUF. Ndio maana, CCM haitalala usingizi hadi hapo itakapohakikisha kuwa inaizika CUF. Hilo halina mjadala. Lakini lenye mjadala ni ikiwa je, CUF itakubali kubwaga chali na kuuliwa kifo cha mende na CCM, baada ya miaka yote hii ya kuhimili vishindo vya ndani na nje yake? Wakati utaamua.
Filed under: Siasa

CCM Zanzibar yapigana vita vya utengano dhidi ya maridhiano
Historia ya Zanzibar itamkumbuka Amani Abeid Karume kama mmoja wa viongozi waliopigania maridhiano, umoja na demokrasia visiwani humo.
Katika kitabu chake Conversation with Myself (Mazungumzo na Nafsi Yangu), aliyekuwa rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini, Marehemu Mzee Nelson Mandela, anaandika:
“Is not our diversity which divides us, it is not our ethnicity or religion or culture that divides us- since we have achieved our freedom – there can only be one division among us: between those who cherish democracy and those who do not.”
Tafsiri isiyo ya moja kwa moja ni kuwa “si mchanganyiko wetu wa rangi unaotugawa, si kabila au dini au utamaduni wetu unaotugawa – tangu tupate uhuru – kunaweza kuwepo mgawanyiko mmoja tu baina yetu: ni kati ya wale wanaoitukuza demokrasia na wale wasiofanya hivyo.”
Katika juhudi za kujenga umoja na maridhiano miongoni mwa Wazanzibari, viongozi wa vyama viwili vikubwa visiwani humo – Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF) walifikia muafaka uliosainiwa na Philip Mangula (wakatui huo Katibu Mkuu wa CCM) na Maalim Seif Sharif Hamad (Katibu Mkuu wa CUF) hapo tarehe 10 Oktoba 2001.

Huu uliitwa Muafaka wa Pili, kwani miaka miwili kabla ya hapo, wakati Salmin Amour Juma akiwa Rais wa Zanzibar, kulikuwa kumefikiwa Muafaka wa Kwanza baina ya vyama hivyo hivyo chini ya uangalizi wa Jumuiya ya Madola, ambao bahati mbaya ulikufa hata haukutumia mwaka.
Kama ulivyokuwa Muafaka wa Kwanza kuchimbukia kwenye uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995, Muafaka wa Pili nao ulitokana na majeraha ya uchaguzi mkuu wa 2000. CUF ilikataa kuyatambua matokeo ya uchaguzi huo na maandamano yake ya mwezi Januari 2001 yakajibiwa kwa mauaji yaliyofanywa na vyombo vya dola.
Wakati huo huo, Karume alikuwa ndiye Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Kwa kile kinachoweza kutafsirika kuwa nia njema na moyo wa uzalendo, serikali yake ikapitisha Sheria Namba 10 ya Mwaka 2001, ambayo iliunda Kamati ya Pamoja ya Rais ya Kusimamia Utekelezaji wa Mwafaka wa Pili.
Kutokana na mapendekezo ya Kamati hiyo, Katiba ya Zanzibar ilifanyiwa marekebisho kupitia sheria inayoitwa Sheria ya Mabadiliko ya Nane ya Katiba ya Zanzibar Namba 2 ya Mwaka 2002, ambayo baadaye ilitiwa saini na Rais Karume tarehe 7 Mei 2002.
Kwa marekebisho hayo, Kifungu cha 66 cha Katiba ya Zanzibar kilifanyiwa marekebisho kwa kuongezwa maneno yafuatayo:
“Isipokuwa kwamba wajumbe wasiopunguwa wawili watateuliwa na Rais kwa kushaurizana na kiongozi wa upinzani katika Baraza la Wawakikishi.”
Mabadiliko haya yalipitishwa katika Baraza la Mapinduzi lililoundwa na CCM watupu na hatimaye yalipitishwa katika Baraza la Wawakilishi lililosheheni pia wawakilishi wa CCM.
Moyo wa Mabadiliko ya Nane ya Katiba ya Zanzibar ulikuwa ni kugawana madaraka kwa lengo la kujenga kuaminiana na maridhiano miongoni mwa Wazanzibari.
Juzi, tarehe 29 Septemba 2016, likisheheni tena wajumbe kutoka CCM, Baraza la Wawakilishi lilifanya Mabadiliko ya 11 ya Katiba ya Zanzibar na kukifanyia marekebisho Kifungu hicho hicho cha 66, ambapo sasa Rais wa Zanzibar halazimiki tena kuwachaguwa “angalau wawakilishi wa wawili kutoka chama cha upinzani.”
Kwa uzoefu wa siasa za utengano zinazochezwa visiwani Zanzibar, mtu huweza kujiuliza ikiwa kulikuwa na umuhimu na ulazima kwa wakati huu kukifanyia marejebisho Kifungu hicho cha 66, wakati CCM imehodhi viti vyote 54 vya uwakilishi, jambo linalowapa uwezo kufanya maamuzi yoyote ndani ya Baraza! Kipi wanachokihofia?
Ukiyaangalia mabadiliko haya kwa undani, utapata jawabu kuwa sio tu wanajaribu kuuvunja msingi wa maridhiano, bali pia kuyaangamiza matunda ya Muafaka wa Pili. Na kama inavyofahamika kuwa kuna Muafaka mwengine wa Tatu wa tarehe 5 Novemba 2009, ambao Wazanzibari wanauiita Maridhiano.
Kwa hivyo, hapana tone la shaka kwamba sio tafauti zetu za kisiasa, kikabila au kidini zinazotugawanya hapa Zanzibar – tangu tulipofikia Maridhiano tarehe 5 Novemba 2009 na kisha kuanzisha muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Agosti 2010 – bali kuna mgawanyiko mmoja tu baina yetu: nao ni kati ya wale wanaoyatukuza maridhiano, umoja na demokrasia na wale ambao wanayapiga vita hayo.
CCM Zanzibar imejipambanua kuwa mpiganaji vita dhidi ya hayo.
Filed under: Siasa Tagged: CCM, cuf, Karume, Muafaka, Zanzibar

“Kimya cha dunia kwa haki ya Wazanzibari chaogofya”
Ukimya wa jumuiya ya kimataifa juu ya suala la uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kwa upande wa Zanzibar kimeanza kuwainua wasomi na wananchi wa kawaida wakihoji dhamira yake.
Uchaguzi huo uliofutwa kinyume na sheria za nchi hapo tarehe 28 Oktoba 2015, siku tatu tu baada ya Chama cha Wananchi (CUF) kukiangusha chama tawala cha Mapinduzi (CCM), ulitajwa na waangalizi wote wa ndani na nje kuwa wa haki zaidi, huru zaidi na wa uwazi zaidi katika historia ya miaka 20 ya chaguzi za vyama vingi.
Sasa ni takribani mwaka wa pili tangu hatua hiyo iliyochukuliwa na CCM kupitia mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha – mwenyewe kada mkubwa wa CCM – na ingawa sehemu kubwa ya wapigakura walioamua kuchagua mabadiliko siku ya tarehe 25 Oktoba 2015 imesalia kwenye matumaini ya utatuzi wa suala hilo chini ya uongozi wao unaowataka wazidi kuvuta subira, uwezekano wa kuendelea kwa subira hiyo si jambo la kuhakikisha.
Soma makala hii iliyoandikwa kwa lugha ya Kiingereza na mwanafunzi wa Sayansi ya Siasa na Mahusiano ya Kimataifa wa Chuo Kikuu cha Nairobi, Kenya, Angela John, akiitahadharisha dunia iliyokaa kimya wakati hali visiwani Zanzibar ikizidi kuvunda.
THE WORLD SILENCE ABOUT ZANZIBAR, A WORRY OR BETRAYAL?
By Angela John, Student of Politics and International relations,
University of Nairobi, Kenya.
The People of Zanzibar have passed through bitter road in the struggle for their Human Rights and complete realization of democracy and rule of law sicne Tanzania has declared multiparty politics in 1992. The champion of this long struggle is the opposition leader in the Isles, Mr. Seif Sharif Hamd, popularly known as Maalim Seif who promised people of Zanzibar that he will fight for Zanzibar even this struggle will cost his life. Maalim Seif and his supporters are fighting nondisappointedly under the very vibrant political party, The Civic United Front – CUF.
CUF has been claiming ridging of Zanzibar election done by rulling party Chama Cha Mapinduzi – CCM through the state organs especially security organs in every general election since the first one in 1995. Violence and human right abuse done by security officers, restricting CUF supporters from vote registration and votting, multiple registration of CCM supporters, non-resident CCM voters, unconstitutional mainlanders registration in Zanzibar election have been Constituting a common election culture in Zanzibar. Despite all those misconducts in elections no scientific, documented evidence was provided by CUF to prove it’s victory in all four past elections, 1995, 2000, 2005 and 2010.
However CUF was technically prepared for the general election in 2015. It not only won the election but it successfully proved it beyond doubt.
Fortunately the International Community witnessed the whole election exercise and it’s outcomes.
Jecha Salim Jecha, claimed to be CCM cadre serving as the Chairperson of Zanzibar Electoral Commission – ZEC annulled the election results unconstitutionally and unilaterally, a decision which is believed to be instructed by the retired President of The United Republic of Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete. Kikwete is accused for ordering armed forces to militarily invade the election results station at Bwawani hotel, thereby paving a good security environment for Jecha’s action to be successful. Despite more than five claims he announced to the public as the base of his decision to annul the election results, he failed to provide at least circumstantial evidence behind his claims.
CUF did a lot to handle the anger of it’s supporters following disappointing Jecha’s decision. CUF leaders restrict it’s supporters from doing any un-lawful actions such as street riots or fighting as the alternative ways to claim their victory. CUF supporters showed high degree of loyalty and obedience to their leaders as they remain calm and silent as instructed. Maalim Seif speaking to the groups of youths at Party’s Headquarters, at Mtendeni street on 28th October, 2015 immediately after election annulment, he said “we know every one of you is very angry but please remain calm and patient. At the moment give us chance to find your democratic right you have showed in ballot box by peaceful methods through negotiations inside the country and with the International Community. If we fail, we will inform you to find your ballot victory with your own methods”.
This article is challenging the seriousness of the International Community on the Zanzibar issue. The 17 months have elapsed while the International Community is showing weak concern on Zanzibar issue. To keep records clear, Zanzibar has no political conflicts between the ruling side and opposition side. The outcomes of 2015 General Election give no indicator of conflict but rather high degree of power abuses and disrespect of democracy and wish of the people done by the rulers. What happened in Zanzibar following 2015 General Elections is the betrayal of people hopes and wishes about their determination, their freedom, their rights and their future and not political crisis at all.
The records show that the world has never hesitate in dealing with dictators. Strong actions have been taken against various dictators all around Africa and around the world at large. However it is very different from Zanzibar perspective. The world is hesitating, delaying and indirectly ignoring the Zanzibar issue. People of Zanzibar are now tired of waiting the International Community. International community should keep in mind that now is high time now for these betrayed people to continue with patience as instructed by their leaders.
Why is International Community delaying to take serious actions against these Tanzania dictators? Two reasons are being brainstormed by Zanzibaris themselves. One is the worry and second is the betrayal. The International Community is thought to have great worry about the new leadership. For longtime Tanzania security officers were given a task to cover the Civic United Front- CUF with the wrong image especially propagandas concerning Islam and Radicalism. The state for long time is producing false reports about CUF to mislead the International Community that CUF is made up of group of radical muslims who emphasize fight against Christianity roots and church dominance in Tanzania.
Has International Community betrayed its own promises of creating democratic world communities? Has the International Community betrayed the people of Zanzibar? Has the International Community failed to Supervise Democracy and it’s principles they brought to Africa. Has International Community betrayed those from opposition side that decided to fight and suffer in defending principles of democracy in land of dictators, Africa?
I advise the International community to be actively concerned with Zanzibar issue before the people especially those disappointed, hungry, betrayed youths have not turned out with their own ways. I advise the International Community to deeply and actively turn to these betrayed people who are struggling under a great respect of peace, order and laws. East Africa is a common land terrorist and terrorist actions. If these youth continue feel being betrayed they will become easily infiltrated by influence from terrorists. If this stage is reached it is not only Zanzibar and Tanzania security that has been endangered but the whole East African region, the interior Africa and the world at large.
Filed under: SIASA Tagged: CCM, cuf, Tanzania, uchaguzi, Zanzibar

Nyerere alivyomtetea Karume Accra
KATIKA mwezi wa Machi hali ya hewa jijini Accra, Ghana, huwa inaudhi bila ya kiasi kwa joto linavyokuwa kali. Jioni ndipo huzidi kushtadi. Nadra mvua kunyesha.
Siku moja Machi 1958, saa za Magharibi, wakombozi wawili wa Kiafrika walikaa, glasi mkononi, wakipunga upepo kwenye baraza ya hoteli ya Avenada, iliyokuwa ikimilikiwa na Mgiriki.
Upande mmoja alikuwa Sheikh Ali Muhsin Barwani kutoka Zanzibar na aliyemkabili alikuwa Mwalimu Julius Nyerere kutoka Tanganyika. Nyerere alikuwa rais wa chama kikuu cha Tanganyika cha kupigania uhuru, Tanganyika African National Union (TANU) na Barwani, akitambulika kuwa kiongozi wa Zanzibar Nationalist Party (maarufu Hizbu) ingawa hakuwa na wadhifa maalum katika chama hicho.
Rais wa Hizbu alikuwa Sheikh Vuai Kitoweo, mzawa wa Jambiani, kwenye mwambao wa kusini mashariki mwa Unguja. Kitoweo alishikilia wadhifa huo tangu alipochaguliwa 1955 hadi mapinduzi ya 1964. Hata hivyo, Barwani ndiye aliyekuwa akionekana kiongozi wa Hizbu hata akapewa lakabu ya “zaimu”, inayotokana na neno la Kiarabu “zaim” lenye maana ya kiongozi.
Wakati huo, Hizbu kilikuwa chama pekee kilichokuwa kikipigania uhuru wa Zanzibar. Chama kingine kikuu, cha Afro-Shirazi Party (ASP), kilikuwa kikipinga Zanzibar isipewe uhuru. Ilifika hadi hata Waingereza walipokubali pafanywe uchaguzi Zanzibar, chama cha ASP kilipinga. Uchaguzi huo ulikuwa wa mwanzo katika Afrika ya Mashariki, ya Kati na kusini mwa Afrika,
Sheikh Shaaban Soud Mponda, Mwafrika aliyekuwa mjumbe wa kuteuliwa katika Baraza la Kutunga Sheria (Legico) alihuzunika na kusema: “Hii ni siku ya giza kwa Waafrika wa nchi hii.” Mponda akiunga mkono ASP.
Mwafrika mwengine kwenye Baraza hilo, Sheikh Rashid Hamadi alimpinga akisema: “Sifahamu vipi katika karne hii ya maendeleo kuwa bado wapo watu wasiotaka uhuru. Haki ya mtu kumchagua mwakilishi wake ni hatua ya mwanzo ya kufikia uhuru.” Hamadi, aliyetoka Ole, Pemba, alikuwa Hizbu.
Siku hizo kaulimbiu ya ASP ilikuwa: “zuwiya”, ikimaanisha uhuru wa Zanzibar uzuiwe. Hoja ya ASP ilikuwa kwamba uhuru ukipatikana utawafaidia Waarabu waliokuwa wamepata elimu zaidi ya Waafrika.
Chama cha ZNP (Hizbu) kiliundwa 1955 na miaka miwili baadaye Februari 5, 1957 Nyerere alisaidia kuasisiwa kwa ASP kwa kuziunganisha African Association na Shirazi Association, jumuiya ya Waafrika na ile ya Washirazi. Chama hicho kilizaliwa kutoka tumbo la ukabila na hata ukunga wake ulikuwa wa kikabila.
Mikono ya wakoloni wa Kiingereza pia ilionekana katika uzalishaji wa ASP. Hilo halikuwa jambo la kushangaza. Waingereza walikwishazoea kufanya mambo kama hayo. Hata Tanganyika mapema 1951, kabla ya TANU kuundwa, wakoloni walimwendea Abdulwahid Sykes na viongozi wenzake wa Tanganyika African Association (TAA), ambayo Nyerere alikuwa mwanachama wake, wakawaambia waunde chama cha siasa kitachokuwa na watu wa makabila mbalimbali.
Sykes na wenzake walikataa kuwa vibaraka wa Waingereza. Waingereza wakamtomeza V.M. Nazerali, Mtanganyika mwenye asili ya Kihindi, na aliyekuwa mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria la Tanganyika (Legico) amwandikie barua Dossa Aziz na kumshauri aunde chama cha aina hiyo. Aziz naye alikataa.
Viongozi kadha wa kadha, wakiwa pamoja na Watanganyika wenye asili ya Kihindi, waliendewa na Waingereza waunde chama wakitakacho wao lakini Waingereza waliondokea patupu.
Kama miaka mitatu baadaye, baadhi ya viongozi hao waliigeuza TAA iwe TANU, chama cha ukombozi. Waliokata uamuzi huo muhimu walikuwa Abdulwahid Sykes, Ally Sykes, John Rupia, Dossa Aziz na Julius Nyerere. Mwandishi Mohamed Said ameandika kwa urefu kuhusu historia hii na jinsi Nyerere alivyowapiku wenzake.
Walipokuwa kwenye baraza ya Hoteli Avenada, Barwani na Nyerere walikuwa wakinywa huku wakizungumzia mustakbali wa nchi zao.
Barwani akinywa maji ya nanasi na Nyerere akipiga vitu vikali kidogo. Barwani alimwambia Nyerere kwamba shida kubwa aliyokabiliana nayo ilikuwa uhaba wa skuli.
“Hatuna skuli za sekondari za kutosha na baada ya sekondari hatuna kitu,” alisema Barwani.
Kwa mujibu wa Barwani, Nyerere alimjibu hivi:
“Miye sihitaji elimu, si kwa sasa. Bahati yangu sina watu wengi waliosoma, kwani ni hao wachache (waliosoma) wanaonipa taabu. Watu kama Fundikira, Lugusha, Marealle, ndio wenye kunipinga. Sitaki wengine zaidi ya hao kwa sasa. Elimu itakuja baada ya uhuru.
“Ninachotaka ni magari ya aina ya Land Rover. Nchi yetu ni kubwa, kubwa sana. Ili tushinde uchaguzi ujao, itatubidi tufanye kampeni nchi nzima. Nitafurahi sana nikipata nchi itayotupa magari ya Land Rover.”
Fundikira aliyemkusudia Nyerere alikuwa Abdallah Said Fundikira aliyekuwa Chifu wa Wanyamwezi wa Itetemya, Tabora. Lugusha alikuwa Chifu Haroun Msabila Lugusha wa Wanyamwezi wa Sikonge, Tabora, na Marealle alikuwa Chifu Thomas Lenana Marealle, aliyekuwa Chifu Mkuu (au Mangi) wa Wachagga wa Marangu, Moshi.
Tunaweza kuandika mengi kuhusu kila mmoja wa waungwana hawa waliokuwa wazalendo lakini tukifanya hivyo tunaweza tukapotea njia na tukatoka kwenye mada yetu.
Mazungumzo hayo baina ya Ali Muhsin Barwani na Julius Nyerere ameyadhukuru Barwani kwenye kitabu cha kumbukumbu zake kiitwacho “Conflicts and Harmony in Zanzibar”.
Barwani na Nyerere walikuwa Accra wakihudhuria sherehe za kuadhimisha mwaka mmoja tangu Ghana iwe huru. Walikuwa wageni wa Nkrumah. Waalikwa wengine walikuwa pamoja na Mallam Aminu Kano (Nigeria), Joseph Murumbi na Tom Mboya (Kenya), Rashidi Kawawa na Paul Bomani (Tanganyika), Kanyama Chiume (Malawi) na Eliradi Mulira (Uganda).
Baada ya kumalizika shamrashamra za maadhimisho hayo, Nkrumah aliwaalika wageni wake nyumbani kwake.
Walipofika, Nkrumah aliwaambia kwamba alikuwa na siri aliyotaka kuwapa. Aliwaeleza kwamba aliwaalika katika sherehe za maadhimisho ya uhuru kama kisingizio kwa sababu akihofia ya kwamba angeliwaambia na mapema sababu hasa ya kuwaalika Ghana, pengine watawala wa kikoloni wangeliwazuia wasisafiri kwenda Accra.
Nkrumah alikuwa na George Padmore, mzawa wa Trinidad, mwandishi na mwanamajumui wa Kiafrika (Pan Africanist) aliyekuwa mshauri wake mkuu wa mambo ya Afrika. Aliwaambia wageni wake kwamba sababu hasa iliyomfanya awaalike Accra ni kuwataka wajadiliane uwezekano wa kuratibu harakati za kuikomboa kila ardhi ya Afrika iliyokuwa chini ya wakoloni.
Nkrumah na Padmore wakawaelezea mpango waliokuwa nao wa kuandaa mkutano mwishoni mwa mwaka huo wa 1958 hukohuko Accra kujadili utumizi wa mbinu za amani, kama zile za Mahatma Gandhi wa India, ili Afrika ijikomboe.
Murumbi, mpiganiaji uhuru kutoka Kenya ambaye siku hizo akiishi Uingereza kwa sababu wakoloni hawakumruhusu aishi Kenya, alisikiliza kwa makini.
Angekuwa Murumbi anaishi Zanzibar ya leo angeingizwa katika kaumu ya wanaoitwa “machotara” na wabaguzi wa Chama cha Mapinduzi (CCM). Angetiwa katika kundi hilo kwa sababu baba yake alikuwa Goa, kutoka India, na mamake alikuwa Mmasai.
Kwa muda mrefu Murumbi alikuwa akisafiria paspoti ya Morocco aliyopewa na babu yake Mfalme Mohamed wa sasa. Alipokuwa London, Murumbi alifanya kazi kubwa ya kuueleza ulimwengu kuhusu madhila yaliyokuwa yakifanywa na wakoloni nchini Kenya.
Siku hiyo alipokuwa Accra nyumbani kwa Nkrumah akimsikiliza kiongozi huyo wa Ghana na mshauri wake Padmore, Murumbi alikuwa na swali lililokuwa likimhangaisha.
Aliuliza: “Tuwaalike viongozi wote, au wale tu tunaowajua kuwa ni wazalendo? Kwani kuna baadhi ya viongozi kama vile wale wa Afro-Shirazi wa Zanzibar wenye kukipinga chama cha Ali Muhsin, na wanajulikana kuwa ni vibaraka wa Waingereza. Tuwaalike nao pia?”
Nkrumah, aliyekuwa amekaa kitini, nusura aruke. Alifoka: “Hapana! Hatuwezi kuwa nao vibaraka!”
Nyerere aliingilia kati kumsaidia rafiki yake kiongozi wa ASP, chama ambacho yeye mwenyewe alisaidia kukiunda.
Alisema: “Nadhani itakuwa jambo la busara zaidi kuwaalika. Watu kama hao si vibaraka kwa imani. Hawajui (mambo). Wakija hapa na kuwa nasi watashajiika kuwa na msimamo wa kizalendo, na hivyo wataiimarisha dhamira yetu badala ya kuidhoifisha.”
Nyerere aliitoa hoja yake kwa ulimi wa asali. Na ilikuwa vigumu wenzake kumpinga. Padmore akatoa rai ya namna ya kulitanzua tatizo hilo.
“Tutauandika mwaliko kwa namna ambayo wakikubali kuja, mabwana zao wa kikoloni hawatokuwa tena na imani nao, na watajikuta peke yao,” alisema Padmore.
Taarifa ya mwaliko wa mkutano huo wa mwisho wa mwaka wa 1958 iliulaani vikali ukabila. Kwa vile ukabila ulikuwa moja ya nguzo za ASP, kama ilivyotazamiwa Karume aliupinga mkutano wa Accra.
Alipopelekewa mwaliko alifanya mkutano mkuu wa hadhara Miembeni, Unguja, na akasema: “Uhuru wetu hautotoka Accra, wala hautotoka Cairo. Utapokuja, utatoka London. Wenye kudai uhuru sasa ni wapumbavu. Hatuwezi hata kutengeneza sindano. Bado tuna miaka mingi ya kujifunza kutoka kwa Waingereza. Tutapokuwa tumekwishajifunza ndipo tutapowaambia waalimu wetu ‘Goodbye’. Sendi popote kutafuta uhuru.”
Karume aligoma. Hakutaka kwenda Accra kuhudhuria Mkutano wa Mwanzo wa Waafrika Wote (All African People’s Conference).
Vuguvugu la Umajumui wa Kiafrika la Afrika ya Mashariki na ya Kati (PAFMECA) liliwatuma Francis Khamisi kutoka Kenya na Kanyama Chiume kutoka Malawi kwenda Zanzibar kusema naye Karume. Baada ya kumbembeleza kwa muda mrefu, hatimaye Karume akakubali kwenda Accra akifuatana na Barwani pamoja na Abdulrahman Babu aliyekuwa katibu mkuu wa Hizbu.
Hatujui pangetokea nini Nyerere angelishindwa kumtetea Karume mbele ya Nkrumah. Gurudumu la historia likishapitia njia fulani huwa muhali, haiwezekani kabisa, kulirejesha nyuma na kulifanya lipite njia nyingine. Likishapita ndo limekwishapita.
Lile la historia ya Zanzibar tangu mwongo wa 1950, kwa kiwango kikubwa, limekuwa likisukumwa na Nyerere.
Tangu aanze kuziingilia siasa za Zanzibar 1957, Nyerere ndiye aliyekuwa akilisukuma gurudumu hilo . Alifanya hivyo kwanza kwa kuzishawishi siasa za ASP na baada ya Aprili 1964 kwa kuidhibiti Zanzibar nzima. Gurudumu alilolisukuma ndilo lililoifikisha Zanzibar hapa ilipo.
Tanbihi: Makala hii iliyoandikwa na mwandishi wa habari mkongwe na mchambuzi wa siasa za kimataifa, Ahmed Rajab, ilichapishwa kwa mara ya kwanza na gazeti la Raia Mwema la tarehe 10 Mei 2017.
Filed under: SIASA Tagged: Ali Muhsin, ASP, Hizbu, Karume, Nyerere, Tanganyika, Uhuru, Zanzibar

Mitizamo miwili ya Nyerere juu ya Israel
WIKI iliyopita niliandika kuhusu mazungumzo waliyokuwa nayo viongozi wawili wa kizalendo wa Kiafrika jijini Accra, Ghana Machi 1958. Viongozi wenyewe walikuwa Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Ali Muhsin Barwani.
Nyerere alikuwa Rais wa Tanganyika African National Union (TANU), chama kilichokuwa kikipigania uhuru wa Tanganyika, na Barwani alikuwa kiongozi wa Zanzibar Nationalist Party (ZNP, au Hizbu), chama pekee kilichokuwa kikipigania uhuru wa Zanzibar kwa wakati huo.
Nilieleza kwamba walipokuwa wakizungumza katika Hoteli ya Aveneda, waliambizana shida zao. Barwani alilalamika kwamba Zanzibar ilikuwa na skuli chache.
Nyerere alimjibu kwa kumwambia kuwa shida kubwa aliyokuwa nayo yeye ilikuwa kupata magari ya kutosha ya aina ya Land Rover ya kufanyia kampeni za uchaguzi Tanganyika nzima.
Nilichozuia kukieleza wiki iliyopita ni kwamba Barwani alitoa rai ya kuziondosha shida hizo mbili kwa mpigo mmoja. Alimshauri Nyerere waende wakaonane na balozi wa Misri ya kimapinduzi hapo Accra.
Barwani alikuwa na hakika wakimueleza shida zao atawasaidia, kwa kumpatia yeye misaada ya elimu na Nyerere magari ya Land Rover.
Nyerere alikubali akamtaka Barwani apange miadi ya kuonana na balozi wa Misri. Agizo hilo Barwani alilitimiza papo hapo kwa kumpigia simu balozi wa Misri na wakakubaliana wakutane siku ya pili saa nne za asubuhi.
Yaliyojiri siku ya pili Barwani ameyaelezea hivi:
“Mapema asubuhi ya siku ya pili rafiki yangu, Nyerere, hakuwako katika chumba chake kilichokuwa kinakikabili changu hotelini. Aliondoka hotelini bila ya kuniachia ujumbe. Kwa hivyo ilinibidi niende peke yangu kwenye ubalozi wa Misri. Nilimwambia balozi kwamba labda rafiki yangu atakwenda mwenyewe, lakini mimi nikihitaji misaada ya masomo ya sekondari na ya baada ya sekondari.”
Sasa tunajua kwamba Nyerere alifanya kusudi kukwepa kwenda kwa balozi wa Misri. Ndiyo maana asubuhi na mapema alimhepa Barwani. Wakati huo Barwani hakuyajua hayo.
Kuna jambo ambalo Barwani alilibania katika kumbukumbu zake alizozimwaga katika kitabu chake “Conflicts and Harmony in Zanzibar.” Ingawa hakulisema wazi jambo hilo, aliliashiria.
Alifanya hivyo alipoandika: “Katika siku zetu zote za mapambano (dhidi ya ukoloni) Nyerere hakuwahi hata mara moja kuhudhuria mikutano ya kupinga ukoloni.” Aliongeza kwamba Nyerere akijua maslahi yake yalikuwa wapi.
Kile ambacho Barwani alibania kukitaja kinaganaga, ni kwamba Nyerere alifanya kusudi asionekane kwa sababu ya woga. Akijua kwamba wakoloni walikuwa wakimuandaa awe kiongozi mtiifu wa Tanganyika huru na hakutaka kuwaudhi.
Labda hiyo ndiyo sababu kubwa iliyomvua Nyerere na shari ya wakoloni. Alikuwa miongoni mwa viongozi wachache wa Kiafrika wasiofungwa na wakoloni au hata kupata misukosuko yao.
Nyerere hakuwa mwiba kwa wakoloni wa Kiingereza kiasi cha kumfunga jela kama walivyomfunga Jomo Kenyatta wa Kenya au Abdulrahman Babu wa Zanzibar.
Ukweli ni kwamba Nyerere alikuwa akipunwa kisiasa na Waingereza. Kwa hivyo, akichelea asijiharibie jina lake kwa kujipeleka kwa Wamisri kama alivyofanya Barwani. Misri ya siku hizo haikuwa Misri ya leo iliyo chini ya mbawa za ubeberu na ukoloni mamboleo.
Misri ya enzi hizo ikiongozwa na Gamal Abdel Nasser aliyekuwa ameisabilia nchi yake kwa ukombozi wa Afrika. Akichukiwa na wakoloni.
Kwa hivyo, siku Nyerere aliyomkwepa Barwani kwenda kwa balozi wa Misri, Nyerere alifanya hivyo kwa akili zake. Akijua akifanya nini. Magari ya Land Rover akiyahitaji lakini hakutaka kufadhiliwa na Misri, adui wa Waingereza.
Akiwa bado mchanga katika harakati za kupambana na ukoloni, Nyerere hakutaka kujiharibia kwa kushirikiana na Misri ya Nasser. Unaweza kusema alikuwa mjanja. Au unaweza kumtetea kwa kusema akijua namna ya kuzicheza karata.
Kulikuwa na sababu maalum iliyomfanya Nyerere asiwakaribie Wamisri. Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel alikuwa mjini. Lililompeleka Accra lilikuwa moja: kukutana na Waafrika wataokuwa viongozi nchi zao zitakapopata uhuru.
Mmojawao alikuwa yeye Julius Kambarage Nyerere. Mwengine alikuwa Ali Muhsin Barwani. Na walikuwapo wengine kutoka sehemu nyingine za Afrika.
Wote walikuwa wamealikwa Accra na Waziri Mkuu Dkt. Kwame Nkrumah kuhudhuria sherehe za kuadhimisha mwaka mmoja wa uhuru wa Ghana.
Kulikuwa na sababu nyingine, iliyokuwa imefichwa na Nkrumah kwa kusudi, kama tulivyoeleza wiki iliyopita lakini kuhudhuria sherehe za uhuru ndiyo iliyokuwa sababu rasmi.
Kuwapo kwa Waafrika hao Accra kuliipa Israel fursa nzuri ya kuwarandia na kuwavutia upande wake dhidi ya Waarabu.
Balozi wa Israel aliandaa karamu ili Waafrika hao wakutane na waziri wake wa Mambo ya Nje. Waziri mwenyewe alikuwa Bibi Golda Meir ambaye miaka 11 baadaye aliibuka kuwa waziri mkuu wa mwanzo wa kike wa Israel.
Barwani alialikwa akutane na Meir hapo Accra. Lakini hakwenda kwenye dhifa hiyo. Nyerere alikwenda.
Nyerere na Barwani walikuwa na mitizamo tofauti kuhusu taifa la Israel. Siku hizo wananchi wa Zanzibar tayari walikuwa na mwamko wa kuipinga Israel na itikadi yake ya Uzayuni. Nakumbuka nikiwa mdogo kuziona kuta za Mji Mkongwe, Unguja, zikichorwa maneno yaliyosema “Hatutaki Masahayuni, Hatutaki Masahayuni”.
Mtoto wa umri kama niliokuwa nao siku hizo, hakuweza kufahamu matamshi hayo yalikuwa na maana gani au na historia gani. “Masahayuni” ndilo jina lililokuwa likitumiwa siku zile kuwaelezea Wazayuni.
Ingawa Barwani alisusa kuhudhuria ile hafla ya balozi wa Israel, hata hivyo alipata habari ya yaliyojiri. Rafiki yake, Mallam Aminu Kano, mwanasiasa kutoka kaskazini mwa Nigeria, ndiye aliyempasha habari hizo. Kano alikuwa kiongozi wa kisoshalisti aliyeongoza vuguvugu dhidi ya ukoloni Nigeria.
Kano alimueleza Barwani nani na nani waliohudhuria karamu hiyo na nini kilichosemwa na nani.
Kwa mujibu wa Kano, Bibi Meir aliwaambia waliohudhuria kwamba alikwenda Accra kusudi akutane na viongozi wa siku zijazo wa Afrika. Aliwaeleza kwamba Waarabu walikuwa wakijaribu kuizingira na kuisonga roho ya Israel. Kwa hiyo, Israel imekuwa na shauku ya kuwa na urafiki na nchi za Kiafrika kuwakabili Waarabu.
Meir aliongeza kwamba Israel ni nchi ndogo na mpya, lakini Waisraeli wana uzoefu wa kuviruka vizingiti. Kwa hivyo, nchi yake ina uwezo mkubwa kwa kuzipa ushauri na misaada nchi za Kiafrika zitazopata uhuru na zitazokabiliwa na changamoto kama Israel ilizokabiliwa nazo.
Golda Meir alikuwa na yake; baadhi ya Waafrika kwenye dhifa hiyo nao pia walikuwa na nayo. Pande hizo mbili zilioneshana moyo wa “nipe, nikupe”.
Nyerere hakuondoka patupu. Pamoja na maakulati na vinywaji alivyokirimiwa, alipata jingine: Waisraeli waliahidi kumpelekea magari aliyoyataka ya aina ya Land Rover ili kukisaidia chama chake cha TANU kiendeshe kampeni za uchaguzi kote Tanganyika.
Na yeye, kwa upande wake, hakufanya uchoyo. Magari hayo yalipowasili Tanganyika alikigaia walau gari moja chama cha Afro-Shirazi katika nchi jirani ya Zanzibar.
Nyerere alipokutana na Golda Meir mjini Accra, Machi 1958, ndipo yalipoanza mahusiano rasmi baina yake na Israel na, baadaye, baina ya Israel na Tanzania. Meir aliwahi kusema kwamba akiuthamini sana mchango wa Israel wa kuisaidia Afrika. Safari moja Nyerere alimueleza Golda Meir kuwa ni “mama wa Afrika”.
Tunaweza kuyagawa mahusiano baina ya Nyerere na Israel au Tanzania na Israel katika vipindi viwili. Katika kipindi cha mwanzo kilichoanza Accra 1958, Nyerere alikuwa amevutiwa na viongozi wa Israel na namna walivyokuwa wamejipangia kuiendeleza nchi yao. Siku hizo Nyerere alikuwa mshirika mkubwa wa nchi za Magharibi. Mahusiano yake na nchi za Mashariki yalianza kwa nguvu baada ya kuundwa Muungano baina ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar Aprili 1964.
Katika kipindi hicho usoshalisti wa Nyerere ulikuwa ukiuigiza ule wa Israel. Hata dhana ya kuanzisha Vijiji vya Ujamaa aliifikiria na kuiendeleza kwa kuuigiza mfumo wa ujima wa kuishi mashambani katika “kibbutzim.” Mfumo, au utaratibu huo, ulizichanganya itikadi za uzayuni na za usoshalisti. Kadhalika, Nyerere alivianzisha vyama vya ushirika kwa kuvisoma vile vya Israel vya “moshavim”.
Labda Nyerere alivutiwa na viongozi wa Kizayuni wa Israel ambao ingawa walianza siasa wakiwa magaidi, lakini itikadi za takriban wao wote, zilikuwa za kisoshalisti. Viongozi hao ni kutoka David Ben Gurion, waziri mkuu wa kwanza wa Israel, hadi Shimon Peres, aliyekuwa kinyonga wa kisiasa na rais wa tisa wa Israel.
Katika kipindi hicho cha mwanzo cha mahusiano baina ya Tanzania na Israel, Nyerere alipata msaada wa Israel kila pale alipotafuta msaada kutoka huko. Hakuona kuwa ni jambo kubwa, au la aibu au la kushangaza kuwa na mahusiano hayo. Lau angelikuwa hai leo sifikiri kama Nyerere angeona kwamba alikuwa na haja ya kutaka radhi kwa kuwa na mahusiano na Israel wakati ule.
Mahusiano hayo mazuri yaligeuka ghafla baada ya Israel kuzishambulia nchi za Kiarabu katika vita ya 1967. Shambulio dhidi ya Misri lilimkera Nyerere bila ya kiasi. Alihisi kwamba aliwajibika kuyavunja mahusiano ya Tanzania na Israel.
Asitosheke bali akawa mbele kuzishajiisha nchi nyingine za Kiafrika ziwe na msimamo kama wake dhidi ya Israel.
Katika hotuba aliyoitoa mara baada ya kumalizika vita ya Mashariki ya Kati ya 1967, Nyerere alisema kwamba sera ya mambo ya nje ya Tanzania imejengeka juu ya misingi ya haki na uhuru.
Tanzania ilikuwa imekwishajitolea kupigania ukombozi wa walioendelea kutawaliwa na wakoloni Afrika na nje ya Afrika, ikiwa pamoja na kuwatetea Wapalestina wapewe haki yao ya kujitawala wenyewe. Hatua hiyo ilimjengea yeye na Tanzania sifa kubwa kimataifa. Ni msimamo alioushika hadi kufa kwake.
Nyerere wa kipindi hicho cha pili cha kutokuwa na mahusiano ya kidiplomasia na Israel ndiye Nyerere anayekumbukwa na kuliliwa wakati huu ambapo nchi yake imeingia katika kipindi kipya cha mahusiano na Israel.
Katika kipindi hiki ni Tanzania nyingine kabisa inayoyafufua mahusiano na Israel. Ni Tanzania iliouacha msimamo wake wa kutoshirikiana na serikali dhalimu.
Wenye kupinga msimamo wa sasa wa Tanzania juu ya Israel wanavunjwa nguvu na baadhi ya nchi za Kiarabu zenye kushirikiana na Israel, kwa uwazi au kwa kificho. Nchi hizo ni pamoja na Tawala za Kifalme za Ghuba (UAE) na Saudi Arabia, inayoshirikiana na Israel katika mikakati ya kuziangamiza Yemen na Syria na kuitishia Iran.
Wenye mtizamo wa kimaendeleo (progressives) wanaendelea kupigwa na butwaa wanapoizingatia misimamo ya sasa ya Tanzania juu ya Israel na juu ya Morocco, nchi ambayo bado inakataa kuipa Sahara ya Magharibi uhuru wake.
TANBIHI: Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza na gazeti la Raia Mwema la tarehe 17 Mei 2017
Filed under: SIASA Tagged: Ali Muhsin Barwani, Israel, Nyerere, Zanzibar

Hivi Magufuli autaka kweli Muungano?
Ni jambo la kawaida viongozi wetu kula viapo vya kuulinda Mungano wa Zanzibar na Tanganyika na huyu Rais John Pombe Magufuli viapo vyake huwa vikali zaidi kwa sababu ya khulka yake ya kujifanya si mtu wa maneno laini.
Wiki kadhaa nyuma katika maadhimisho ya miaka 53 ya Muungano wa nchi hizi mbili yaliyofanyika Dodoma, Rais Magufuli alisema: “Nataka niwahakikishie kuwa tutaulinda Muungano kwa nguvu zote, na kamwe asijitokeze mtu yeyote atakaye jitahidi au kujarbu kuuvunja muungano, atavunjika yeye.”
Kauli hizi usidhani ni za masikhara. Kisa cha viongozi wa Uamsho kuendelea kusota ndani ni kutumia haki yao ya kisheria kuuhoji uhalali wa Muungano, kupinga na kuukataa unyonyaji ulio katika Muungano huo, wakiamini hauna maana bora tu uvunjike.
Kilichofuata ni kubambikiziwa kesi ya ugaidi isiyo na kichwa wala miguu, ikikosa ushahidi kwa miaka minne sasa, imekuwa ni hadithi ya kupigwa dana dana kila siku.
Kwa hiyo, hata ukihoji Muungano kwa kutumia haki yako ya kikatiba, matokeo yake utavunjika, utateketea, uvurugike na kuumia. Ukiacha yanayowakumba Uamsho, mifano hai mingine ipo mingi tu.
Jambo moja linaloumiza na kushanganza mno na ambalo ndio msingi wa makala hii ni kwa nini viapo visiwe kutatua hizi shida, matatizo, na unyonyaji ambavyo vipo katika Muungano?
Ningemuona Magufuli ana nia njema na Muungano kama angekula kiapo akisema: “Nataka niwahakikishie tutaondoa unyonyaji na kero zilizo katika Muungano huu kwa nguvu zetu zote, na kamwe asijitokeze mtu kuvunja juhudi zetu kwa sababu atavunjika yeye.”
Kipi cha msingi kati ya kula viapo na kulinda Muungano wenye chungu ya malalamiko na kero au kutumia gharama zote kufuta hizi kero na matatizo ya Muungano huo?
Kuulinda Muungano, ambao unajuwa wazi una unyonyaji ndani yake, ni sawa na kumshinikiza mwanamke aishi na wewe kama mke na mume wakati ndoa yenu imejaa matatizo na hasara na mmeshindwa kuyaondosha kwa nusu karne ya ndoa yenu.
Ukimuuliza mwanandoa yeyote, lipi bora kati ya kulinda kwa nguvu zote ndoa yenye matatizo au kutumia nguvu zote kuondoa matatizo, ni wazi kila mwenye akili atatumia nguvu kufuta matatizo yaliyo kwenye ndoa, kwa sababu ndoa isiyo na unyonyaji na manyanyaso haihitaji viapo, kutishana wala nguvu za ziada kuilinda.
Hapa maana yake ni kuwa Muungano wa usawa kwa pande zote, wala hauna haja ya vitisho au vifaru na mitutu kuulinda. Wananchi wa pande zote wataulinda, kuuenzi na kuupenda kwa sababu hauwanyonyi, wala rais hatokuwa na kazi ya kula viapo na kutisha majukwaani kuulinda.
Muungano unaolindwa kwa maneno makali na vifaru na majeshi, ni kiashiria kuwa wananchi hawatendewi haki katika kuamua lipi wanalitaka na lipi hawalitaki, hulazimishwa kulitii hata lile wasilolifurahia.
Husikii viongozi wakila viapo kutumia nguvu kufuta unyonyaji ulio katika Muungano, bali wote kipau mbele chao kuulinda Muungano wenye unyonyaji.
Ndio maana kero za kufyonzana katika Muungano zimebaki kwa nusu karne sasa, ambapo Mambo ya Muungano yalikuwa kidogo sana lakini yakaongezwa kinyemela hadi yakawa mengi, na ndipo unyonyaji ukazidi kukuwa.
Kwa nusu karne hii, kama kila viongozi wangekuwa wanatumia nguvu zao kuhakikisha Muungano haunyonyi upande wowote,naamini leo tungekuwa na Muungano unaopendwa na kila upande, au ambao ungechukiwa na wachache sana kama wangekuwepo.
Awadh Ali Said, mwanasheria kutoka Zanzibar anapozungumzia matatizo ya Muungano katika muktadha wa mapato anasema suala la mapato “linaingia katika suala la uchumi, lakini uchumi si suala la Muungano.”
Kichekesho ni kuwa kila mmoja kati ya Tanganyika na Zanzibar ina uchumi wake na mzigo wa kushughulikia, ikiwemo miundombinu, umeme, elimu, maji safi, “lakini nyenzo kuu za uchumi ambazo ni sera za fedha, sera za kodi, benki kuu, yote hayo yako upande mmoja (Tanzania Bara)”, anasema mwanasheria huyo.
Hii ni sawa na kuiambia Zanzibar kuwa: “Uchumi ni wako lakni huna udhibiti wa sarafu yako, huna udhibiti wa sera za kodi na huna uwezo hata wa kukopa lakin mwenzako muliyeungana amedhibiti yote hayo”, kwa mujibu wa mjumbe huyo wa zamani wa Tume ya Katiba, maarufu kama Tume ya Warioba.
Unyonyaji wa Muungano hata wakereketwa wa Chama cha Mapinduzi (CCM) hulalamika wanapoona maji yamezidi unga. Mwezi Mei mwaka jana, Mbunge wa CCM wa Jimbo la Kijito Upele, Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha, alilalamika Bungeni akisema:
“Tumezungumza kwa muda mrefu suala la kugawana mapato kati ya serekali ya mapinduzi Zanzibar na ya Muungano…naomba suala hili lifike mwisho limalizwe.”
Unagundua kuwa kumbe ni Muungano ambao kwa muda mwingi umekuwa ukinyonya upande mmoja. Mbunge wa Singida Mjini, Tundu Lissu, amekuwa mara kwa mara akiulalamikia muungano huu wa kinyonyaji hadi kufikia kusema kuwa “Zanzibar imegeuzwa kuwa koloni la Tanganyika.”
Suala la kila nchi kuwa na nyenzo zake kamili za mapato ambalo Awadh alilizungumzia, lilikuwa limewekwa sawa katika Rasimu ya Katiba Mpya iliyopendekezwa.
Bahati mbaya katika Bunge Maalum la Katiba kujadili rasimu ile, wabunge wengi wakiwa wa CCM na wengine kutoka makundi tofauti ya kijamii, wakageuza mambo na hali ikarudi kama mwanzo (unyonyaji).
Kila kitu ambacho kilionekana kinaleta ukakasi katika Muungano kiliwekwa sawa kwa mujibu wa maoni ya wananchi, lakini bahati mbaya hata ule mfumo wa serikali tatu uliopendekezwa nao wakaukata roho.
Kwa nusu karne yote hii, ni wazi kuwa watawala wanalazimisha tu Muungano hu uendelee kubaki.
Tangu awali ilishaonekana wazi kuwa Rais Magufuli hakuwa na nia njema na maridhiano kwenye Muungano, hasa pale aliyekuwa waziri wake wa katiba nba sheria, Dk. Harrison Mwakyembe, alipoutambulisha umma kuwa mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya hakikuwa kipaumbele kwa Rais Magufuli.
Wakati akiondoa uwezekano wa kusaka maridhiano kwenye muundo wa Muungano, Rais Magufuli anazidisha vitisho, akipuuzia ukweli kuwa Muungano wenye ridhaa utalindwa na wananchi wenyewe. Hakuna anayeweza kuizuwia hasa nguvu ya wananchi hao, endapo wataamua kiudhati na kiukweli kuwa wanataka kuuvunja.
Ili kuufanya Muungano huu kuwa na afya na ubaki imara kwa pande zote, la muhimu ni kuutoharisha ili usiwe na harufu ya dhulma za upande mmoja dhidi ya mwengine.
Ili Magufuli aonekane na nia njema na Muungano, basi kwanza airudishe rasimu ya katiba mpya, tena ile ambayo wananchi waliipendekeza. Kwa hatua hiyo, panaweza kupatikana katiba itayofuta kero zote, kwa sababu kutisha watu na kuwasweka ndani wanaousema Muungano huu, hakuuimarishi Muungano wenyewe.
Makala hii kwa mara ya kwanza ilichapishwa katika gazeti la MwanaHalisi la Jumatatu, Mei 8 -14, 2017. Hapa imehaririwa upya.
Filed under: SIASA Tagged: Magufuli, Muungano, Tanganyika, Tanzania, Uamsho, Zanzibar

Ulipumba unadumaza demokrasia
KATIKA siasa za Tanzania kuna kupakaziana kwa kila aina, walio madarakani huwakazia wa upande ule wanaoitwa wapinzani. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kiliitwa chama cha Wachaga kwa sababu mwaasisi wake ni Eddwin Mtei.
Hawakusema lolote kwa aliyekuwa Makamu wake, Bob Makani (marehemu) ambaye ni Msukuma wa Shinyanga. Baadaye siku zilivyokuwa zinasogea na Chadema kushika moto Kanda ya Kaskazini, wa upande wa pili wakasema chama cha ukanda kupitia Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa, Mwenyekiti Freeman Mbowe.
Ujio wa waliokuwa mawaziri wakuu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye, ukatafsiriwa, wakipewa nchi ni hatari na kwamba wataigawa nchi kikanda. Nadhani ni kutokana na mtazamo huo, Freeman Mbowe akamteua Dk. Mashinji Msukuma kutoka Kanda ya Ziwa, ili kuifuta ile dhana ya Chadema kuwa chama cha Ukanda wa Kaskazini.
Kwa upande wa Chama cha Wananchi (CUF), wa upande ule wakadai kuwa ni chama chenye udini; chama cha Waislamu, huku wakijua fika kwamba Sheria ya Vyama vya Siasa inakataza na katika katiba ya chama hicho, hakuna mahali unatajwa uislamu.
Kule Unguja wa upande ule wakasema CUF ni chama cha Wapemba. Ninavyojua mimi hakuna kabila hapa Tanzania linaloitwa Wapemba. Mbona hakuna Wambeya!
Kama hiyo haitoshi, wakaongeza sifa mbaya nyingine kwamba CUF kikipewa kushika madaraka Zanzibar, kitarudisha usultani eti CUF kina nasaba na uwarabu na ikasanifiwa kwamba Waarabu walioikimbia Zanzibar, ndio wanaotoa fedha za kuendesha chama hicho.
Mwaka 2015 kuelekea Uchaguzi Mkuu, vyama vya upinzani vilijiunga pamoja na kuazimia kumsimamisha mgombea mmoja kama mkakati wa kukiondoa madarakani Chama cha Mapinduzi (CCM), ikazaliwa Ukawa (Umoja wa Kutetea Katiba ya Wananchi), umoja ambao uliundwa kutokana na kupinga jinsi Bunge la Katiba lilivyokuwa likiendeshwa na Spika Samuel Sitta (marehemu), alikuwa anapendelea wajumbe wa chama tawala. Vyama vya upinzani vikaamua kususa Bunge na imeelezwa jina la Ukawa aliliibua Profesa Ibrahim Lipumba ambaye pia alikuwa mjumbe kwa tiketi ya CUF na alikuwa na kofia ya Mwenyekiti wa chama hicho.
Viongozi wakuu wa Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na National League for Democracy (NLD), wakaita mkutano mkubwa uliofanyika pale Jangwani, Dar es Salaam na wakatiliana saini ya kuungana kuipinga CCM. Prof Lipumba ndiye aliyekuwa Mwenyekiti wa wenyeviti na alishiriki kikamilifu katika mazungumzo ya kumkaribisha Lowassa Ukawa.
Ujio wa Lowassa na kuteuliwa kwake kuwa mgombea wa nafasi ya urais, kulizima ndoto ya Prof Lipumba ambaye tayari chama chake cha CUF kilikuwa kimemteua kugombea urais. Yako mengi yaliyosemwa kwamba Lipumba na Dk. Slaa walirubuniwa na kuahidiwa kula vinono kama watajiuzulu uongozi. Mkakati huu ulifanikiwa, lakini haukudhoofisha dhamira ya Ukawa. Lipumba na Slaa waliondoka nchini; mmoja akadai anaenda kufanya utafiti Rwanda, mwingine akaenda Marekani na baadaye Canada.
Prof Lipumba aliandika barua ya kujiuzulu nafasi yake ya Mwenyekiti na aliondokea hotelini alipofanyia mkutano na wanahabari kwenda kupanda ndege Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam. Ukawa wakapata pigo jingine kubwa kwa kuondokewa na Mwenyekiti wa NLD, Dk. Emmanuel Makaidi, lakini waliendelea kupigana na kukamilisha ‘vita’ vya Uchaguzi Mkuu Oktoba, mwaka 2015.
Miezi minane baadaye, Lipumba akarejea nchini. Akawashangaza wenzake aliposema hataunga mkono Ukawa, umoja alioshiriki kuunda. Kama hiyo haikutosha, akaenda Ikulu kumwona Rais John Magufuli na kumpongeza kwa ushindi, ingawaje CUF kama chama walikuwa wanapinga kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi Zanzibar. Walioelewa hili walielewa.
Miezi michache baadaye, Lipumba akaandika barua kwa Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad, akieleza kwamba anafuta barua yake ya kujiuzulu na anataka kurejea kwenye nafasi yake ya uwenyekiti. Barua yake ya awali ilikuwa haijajibiwa kwa sababu chama kilikuwa kwenye harakati za uchaguzi, yeye akachukulia kwamba kwa vile hakujibiwa, basi ana haki ya kuendelea kuwa Mwenyekiti!
Walioelewa wameelewa baada ya Lipumba kuvamia mkutano mkuu na kujisimika uwenyekiti. Hapo ndipo mimi nasema sitaki ulipumba, unadumaza demokrasia na watu wote wenye uelewa hawapendi ulipumba, unavuruga chama ambacho umetoka nacho mbali, unashirikiana na polisi ambao kabla ya Uchaguzi Mkuu walikupiga virungu, wakakusweka ndani na kukufungulia kesi katika Mahakama ya Kisutu. Leo ndio maswahiba wako, wanakupa jeuri ya kuvamia ofisi za chama, kuwapiga na kuwajeruhi wale ambao hawakubaliani na ulipumba wako!
Hili liwe fundisho kwa viongozi wa vyama vingine kwamba visifanye ajizi ya kumwaminisha mtu mmoja kwamba bila yeye mambo hayaendi. Anzeni kupeana kijiti cha uongozi kama wanavyofanya wale wa chama cha dola. Chama ni cha wanachama, hata kama wewe ndiye uliyekianzisha na viongozi wasimilikishe uongozi. Kuna vyama vina viongozi wale wale toka vianzishwe na vimekwishapoteza uhalali wa kuitwa vyama vya siasa, lakini vinalelewa tu kwa sababu iko sababu ya kuviacha vidumae na kudumaza demokrasia.
Na hivi ndivyo ilivyo kwamba chama tawala kinafurahia wapinzani wakivurugana. Kuna chama hakina hata mwakilishi ngazi ya kijiji/kitongoji. Chama kiko mfukoni hakina hata ofisi na kimeshindwa kupata hata diwani mmoja, lakini vinatoa matamko ya kuvipinga vyama vyenye uwakilishi bungeni!
Tanbihi: Makala hii ya Balinagwe Mwambungu imechukuliwa kutoka mtandao wa gazeti la Mtanzania kupitia kiungo: http://mtanzania.co.tz/ulipumba-unadumaza-demokrasia/
Filed under: SIASA Tagged: cuf, Lipumba, siasa, Tanzania

La mchanga na uovyo wa Muhongo
Filed under: SIASA Tagged: Magufuli, mchanga wa madini, Muhongo
